Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi kwa kumteua Andrew Massawe kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Sambamba na hilo, pia Rais amemteua Profesa Ulingeta Mbamba, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kipindi cha miaka mitatu.
Prof Ulingeta ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Biashara, pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade).
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo Jumatano, Aprili 5, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Zuhuru Yunus.
Uteuzi wa Dk Mbamba anachukua nafasi ya Profesa Blasius Nyichomba, ambaye amemaliza muda wake.
Kwa upande wa Massawe taarifa hiyo imeeleza ameteuliwa ili kujaza nafasi ya Dk Tausi Kida aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Uwekezaji.
Masawe kabla ya uteuzi huo aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, nafasi aliyeteuliwa Aprili mwaka 2021.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo umeanza Machi 29, 2023.
Uteuzi huu unakuwa wa pili kufanyika ndani ya mwezi Aprili. Mwezi Aprili 3,2033 Rais Samia alifanya mabadiliko kwa mabalozi wawili na uteuzi wa balozi mmoja.
Katika uteuzi huo alimteua Yacoub Mohammed kuiwakilisha Tanzania katika Falme za Kiarabu (UAE). Kabla ya uteuzi huo, balozi Mohamed alikuwa balozi wa Tanzania nchini Uturuki..
Pia katika uteuzi huo alimpangia Balozi Humphrey Polepole kuiwakilisha Tanzania nchini Cuba, kabla ya uteuzi huo, Balozi Polepole alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Aidha alimteua Iddi Seif Bakari kuwa balozi na kumpangia ubalozi nchini Uturuki.Kabla ya uteuzi huu, Bakari alikuwa Konseli Mkuu nchini Dubai.