Waislamu matala waungana kukemea vitendo vya ushoga

Na Zulfa Mfinanga 

Moshi.

Waumini wa Dini ya kiislamu wa Kijiji cha Matala wilayani Moshi vijijini katika Mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kuungana na waislamu wengine duniani kulaani na kukemea vitendo vya ushoga na ulawiti vinavyoendelea ndani ya jamii kwa kuwa vinaenda kinyume na maandiko Matakatifu ya Mwenyezi Mungu.

Akizungumza na baadhi ya waumini wa Dini hiyo leo kijijini hapo, Sheikh wa Msikiti Mkuu wa BAKWATA Matala Ibrahimu Idd Tarimo amesema ni wakati sasa wa kupinga kwa vitendo tabia hiyo haramu na kwamba amewataka waislamu wote kujumuika na waislamu wenzao kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa huo tarehe 8 mwezi Aprili mwaka huu mjini Moshi kwa ajili ya kufanya maandamano ya amani ya kulaani vitendo hivyo.

“Ndugu zangu hali ni mbaya kwenye jamii zetu, kwenye familia zetu na kwenye Mkoa wetu, sisi kama waislamu tuliopewa dhamana ya kuhakikisha kuwa jamii ya kiislamu inaishi kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu hatuna budi kuchukua hatua mapema Ili kunusuru kizazi chetu” alisema Sheikh Ibrahimu 

Aidha aliwataka waumini wote kushiriki kikamilifu katika maandamano hayo ya amani na halali yenye lengo la kuonyesha kuchukukizwa na vitendo hivyo haramu Ili kuhakikisha Serikali kwa kushirikiana na jamii inatokomeza kabisa matendo haya maovu ndani ya jamii.

Kwa upande mwingine Sheikh Ibrahimu aliwataka wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika misingi ya dini ya Kiislamu ili wawezi kutambua mambo mema yaliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu na mambo mabaya yakiwemo ushoga na ulawiti yaliyokatazwa na kulaaniwa na Mwenyezi Mungu.