Na Mapuli Misalaba,
Shinyanga
Kuelekea kilele cha
maadhimisho ya siku ya Maji Duniani baadhi ya wananchi katika Manispaa ya
Shinyanga wamepongeza huduma zinazoendelea kutolewa na Mamlaka ya maji safi na
usafi wa mazingira Manispaa hiyo SHUWASA
huku wakitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Wananchi hao wametoa
pongezi hizo leo wakati wakizungumza na Misalaba
Blog kwa nyakati tofauti kuelekea maadhimisho hayo.
Wamesema kuwa wanaendelea
kupata huduma ya maji lakini bado zipo changamoto zinazohitaji ufumbuzi ili
kuwasaidia wananchi kuendelea kunufaika na huduma hiyo na kwamba wameiomba
Mamlaka hiyo kuboresha zaidi huduma ya maji safi na salama kwa wananchi sambamba
na kutatua changamoto ya bili za maji.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano na mawasiliano kutoka Mamlaka
ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Shinyanga SHUWASA, Bi Nsianeli
Gerald amewataka watumiaji wa huduma hiyo
kutoa taarifa pale inapotokea changamoto
ili ishughulikiwe haraka.
Akizungumzia siku ya maji
Duniani Bi Nsianeli amesema mamlaka hiyo tayari imefuta faini za wateja
waliokatiwa maji na badala yake watalazimika kulipa madeni yao kwa makubaliano.
Kesho ni kilele cha
maadhimisho ya wiki ya maji Duniani ambayo ilizinduliwa rasmi Machi 16, Mwaka
huu ikiongozwa na kaulimbiu inayosema “kuongeza
kasi ya mabadiliko katika sekta ya maji kwa maendeleo endelevu ya uchumi”.