Simba maarufu katika hifadhi ya Serengeti, Bob Junior ambaye ameuawa na wenzake hivi karibuni, enzi za uhai wake akiwa katika maisha yake ya kawaida ndani ya hifadhi ya Serengeti. |
Na Claud Gwandu, Arusha
MSAKO mkali unaendelea katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kumtafuta Simba aitwaye Joel ambaye ni kaka yake Simba maarufu Bob Junior aliyeuawa na wenzake mwishoni mwa wiki iliyopita mashariki mwa hifadhi hiyo.
Bob Junior aliuawa na simba wenzake wanaokadiriwa kuwa kati ya watatu hadi watano Machi 11, 2023, katika mapambano ya kugombea uongozi wa kundi na mwili wake uliliwa na wanyama wengine walao nyama wakiwamo Fisi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamishna wa Uhifadhi katika Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA), William Mwakilema, alisema simba Joel alikuwa na kaka yake wakati wa mapambano hayo lakini hajaonekana tangu jumamosi.
“Kutokana na umaarufu wa Simba hao ambao walikuwa kivutio kikubwa kwa watalii, tunataka kujua hatma yake na ikibidi tumweke katika uangalizi maalum, na ndio maana operesheni ya kumtafuta inaendelea,” alisisitiza Mwakilema.
Alifafanua kuwa mapambano ya kugombea uongozi katika makundi ya wanyama ni jambo la kawaida, na kabla ya hapo kulikuwa na majaribio kadhaa ya kumng’oa Bob Junior na mwenzake Joel, lakini hayakufanikiwa.
Alisema kuwa Bob Junior anayekadiriwa kuzaliwa mwaka 2010 na hivyo kuwa na miaka 12 alijipatia umaarufu kutokana na ukubwa wa umbile lake na kuwa na nywele nyingi nyeusi zilizofananishwa na za mwanamuziki maarufu wa Jamaica, Bob Marley.
“Ukubwa wake kutokana na vinasaba na wingi wa nywele alizokuwa nazo, vilimfanya kuwa kivutio kwa watalii waliompachika jina la Bob Junior wakimaanisha kuwa ni mdogo wake Bob Marley, mwanamuziki aliyekuwa akifuga rasta,” alisema Mwakilema na kuongeza:
“Ni bahati mbaya mwili wake uliliwa na Wanyama wengine walao nyama hasa Fisi, tumepoteza fursa ya kuweka kumbukumbu yake na ndio maana tunamfatuta kaka yake Joel ambaye walikuwa naye wakati wa mapambano na kundi la vijana waliotaka uongozi wa kundi,” alieleza Mwakilema.
Tukio hilo,kwa mujibu wa Mwakilema lilitokea katika eneo la Namiri lililopo mashariki mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alikokuwa anaishi Bob Junior na familia yake akishirikiana na kaka yake Joel.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI) Idadi ya Simba katika mfumo wa ikolojia ya Serengeti, ambao huishi katika familia, inakadiriwa kuwa kati ya 3,000 na 3,500.
Bob Junior akiwa ameuawa |
Utafiti uliofanywa na TAWIRI unaonyesha kuwa Mfumo wa ikolojia ya Ruaha-Rungwa ndiyo inayokadiriwa kuwa na simba wengi nchini na duniani kote.