NA ZULFA MFINANGA, ARUSHA
Vitendo vya ukatili wa kingono nchini vinazidi kushika kasi huku kundi la watoto likitajwa kuwa waathirika wakubwa wa vitendo hivyo jambo lililopelekea wanaharakati wa ukatili wa kingono pamoja serikali kutoka wilaya ya Meru mkoani Arusha kushirikiana katika kupambana navyo.
Awali jamii ya Kata ya Maruvango iliyopo wilayani humo ilikuwa ikitatua changamoto za ukatili wa kingono kimila maarufu kama muroo, hali iliyopelekea kuongezeka kwa vitendo hivyo zikiwemo mimba na ndoa za utotoni, ubakaji pamoja na vipigo kwa wanawake.
Kufuatia hali hiyo mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kushirikiana na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya kitongoji hadi Kata, ustawi wa jamii, polisi kata, dawati la jinsia-polisi kutoa elimu kwa jamii hiyo hali iliyopelekea kuweka maazimio yaliyokataza kutatua kesi zote za kijinai kwa njia ya kimila na badala yake kesi zote zinazohusiana na jinai zitatuliwe kwa kuzingatia mifumo ya kisheria.
Baada ya elimu hiyo hali ya utoaji wa taarifa kwa vyombo vya dola umeimarika licha ya matukio ya ubakaji kuendelea kuripotiwa jambo lililowalazimu wanaharakati kwa kushirikiana na serikali kutoa elimu katika shule ya sekondari Maruvango iliyopo wilayani humo juu ya kujilinda na kuripoti viashiria na vitendo ya kingono ikiwa ni pamoja madhara yake.
Akizungumza na wanafunzi hao, Askari Kata ya Maruvango Inspekta Sai Nteminyanda amewataka vijana hao kutambua sehemu sahihi za kuripotia matukio hayo pamoja na sehemu hatari zinazochochea matukio hayo huku akiwaondoa woga kwa kuwataka kutumia ofisi za serikali kutoa taarifa pale wanapokutana na viashiria vya ukatili wa kingono.
“Ukatili wa kingono hauji bila viashiria, ni vyema mkavitambua ili kuweza kutoa taarifa mapema kabla ya tatizo halijatokea, na niwaambie kuwa ofisi za serikali kuanzia ngazi ya kitongoji hadi Kata zipo kwa ajili yenu, ingieni mtoe taarifa, lakini pia hapa nimewafundisha maeneo salama ya kutembea, kwa mfano kutumwa usiku, hata kama ni mzazi kakutuma jaribu kumuelewesha madhara ambayo yanaweza kutokea” Alisema Inspekta Sai.
Mkurugenzi wa Shirika la Community Economic Develepment and Social Transformation (CEDESOTA) Jackson Muro amesema ni wajibu kwa wanafunzi kupasaza sauti kupinga vitendo hivyo, kujilinda kwa kushiriki katika michezo pamoja na kujiunga na vilabu mbalimbali za kitaaluma ili kupata mawazo mapya huku akiwasisitiza kuwafichua wanaofanya vitendo hivyo na kuwaficha wanaotendelewa ili kutunza heshima na utu wao mbele ya jamii.
“Njia nyingine za kuepuka vitendo hivyo ni pamoja kuepuka kupokea zawadi kutoka kwa watu wasioaminika……na niwasihi msione aibu kuzungumza masuala haya kwani nyie ni viongozi watarajiwa, kwa hiyo hamna budi kuhakikisha mnaishi kwenye mazingira salama ili kutimiza ndoto zenu na pia mtumie namba 116 kupiga simu bure kutoa taarifa ya vitendo hivyo” Alisema Muro.
Kwa upande wake mwanaharakati wa kujitegemea Evarester Mlamie alitaka wanafunzia hao kutunza miili yao ili isiwe rahisi kwa mtu yeyote kuishika shika kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamejiepusha na viashiria vya ubakaji.