Alawiti wanafunzi 18, atiwa mbaroni

 Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mkazi wa kijiji cha Komela, wilayani Moshi mkoani hapa, Shukuru Nguma kwa tuhuma za kuwalawiti kwa nyakati tofauti wanafunzi 18 wa shule tofauti za msingi kijijini hapo.


Nguma anadaiwa kuwalawiti wanafunzi hao wa kiume ambao ni kuanzia darasa la kwanza hadi la tano kwa kuwapa pipi na fedha.

Akizungumzia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda alisema kijana huyo alikamatwa Januari 21, baada ya kuzagaa kwa taarifa hizo ambapo timu ya uchunguzi ilitumwa kijijini hapo kujiridhisha na kubaini ukweli wa tuhuma hizo.

“Huyu mtuhumiwa tayari tunaye, tumefuatilia tumebaini ni kweli baada ya kutuma timu yetu kuchunguza na Serikali tayari imeshachukua hatua, ikiwemo kumkamata, kwa ngazi ya wilaya tumeshakamilisha taratibu zote ili tumfikishe mahakamani,” alisema.

Kayanda alisema kijana huyo sio mara yake ya kwanza. Akiwa na miaka 17 aliwahi kukamatwa na kuhukumiwa kifungo cha nje.

“Yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya namna hiyo kwa watoto wetu wa shule, iwe chekechea, shule ya msingi au sekondari hatutamwacha, tutamkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, ili tukomeshe tabia za namna hii ambazo hazifai katika jamii yetu,” alisema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa aliungana na mkuu huyo wa mkoa akisema kuna taratibu zinaendelea ikiwemo kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo.

“Ni kweli mtuhumiwa huyo anashikiliwa katika kituo cha Polisi Himo na taratibu za kisheria zitakapokamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Maigwa.


Via: Mwanachi