* Yawaepusha wananchi kufuata huduma hiyo umbali wa Km89
Na Mwandishi Wetu
BAADA ya Bohari ya Dawa (MSD) kupeleka mashine za picha za mionzi (X-Ray) katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze, hatimaye wakazi wa Wilaya hiyo wameepushwa na adha ya kusafiri umbali wa kilometa 89 kufuata huduma hizo.
Kabla ya huduma hizo katika hospitali hiyo, wagonjwa 15 hadi 20 kwa mwezi walikuwa wanapewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Tumbi mkoani Pwani na hivyo kumsababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Hayo yamesemwa na Mfamasia wa Hospitali ya Wilaya ya Chalinze-Msoga mkoani Pwani Shaaban Kinesi alipokuwa akitoa taarifa ya uboreshwaji wa huduma za matibabu mbele ya maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD) walipotembelea hospitali hiyo.
Kinesi amesema kwamba kutokana umbali huo, wa kufuata huduma ya X- Ray ulisababisha changamoto kubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Chalinze na maeneo na kufafanua kwa Sasa wameanzisha huduma hiyo kwenye hospitali hiyo,hivyo kupunguza umbali wa kufuata X-Ray.
“Hapo nyuma tulikuwa tunapata wagonjwa wa huduma za mionzi lakini tulikuwa tunawapa rufaa ya kwenda Tumbi ambapo kuna umbali wa kilometa 89.Hiyo ilikuwa inasababisha gharama na kupoteza muda mwingi kwa mgonjwa lakini MSD imetuletea huduma hizi zinapatikana katika hospitali ya Msoga,” amesema.
Ameongeza kwa sasa katika hospitali hiyo kuna mashibe za X-Ray mbili na zote zinatoa huduma, na kwamba kama hospitali ya Wilaya wanaishukuru Bohari ya Dawa kwa kuwapatia X-ray hizo ambazo kwa sehemu kubwa zikekwenda kuondoa changamoto ya muda mrefu.
Aidha amesema mbali ya kupata X- Ray hizo pia wamepatiwa majokofu kwa ajili ya chumba cha kuhifadhia maiti, mashine ya usingizi, vitanda na magodoro pamoja na vifaa vingine muhimu ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa.
Kuhusu upatikanaji wa dawa, Mfamasia huyo alisema kwa upande wao hali inaridhisha kwani dawa zote muhimu kutoka MSD zinapatikana kutokana na kuzingatia vigezo wakati wa maombi.
Kwa upande wake, Ofisa Huduma kwa Wateja Kanda ya Dar es Salaam, Mfamasia Diana Kimario alisema mahitaji yote muhimu yanaendelea kupelekwa kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa kwa wananchi.
“MSD tumekuwa tukishirikiana na Hospitali ya Chalinze tangu ikiwq Zahanati baadae kituo cha Afya na sasa Hospitali ya Wilaya.Tutaendelea kushirikiana na uongozi wa hospitali hii ikiwa pamoja na kuwapatia dawa ,vifaa tiba na vitendanishi vyote ambavyo wataomba kwetu,”amesema Kimario.