Afyaplus yatoa mashine za kutengeneza taulo za kike za bure mashuleni iringa

 

SHIRIKA  lisilo la kiserikali la afya Plus kupitia mradi wa maabara ya Hedhi salama unao lenga kuondoa vikwazo  wanavyovipata binti wakati wa hedhi wakiwapo shule  limetoa msaada wa mashine 15  na vifaa vya kuzalishia  taulo za  kike  shuleni kati ya mashine 50 zitakazotolewa Kwa shule lengwa mkoani Iringa .


Akitoa taarifa   ya  mradi  huo wakati  wa kukabidhi mashine  hizo jana  ,mkurugrnzi wa shirika la Plus Suzan Yumbe  alisema  kuwa   kutokana na  tafiti  ambazo  shirika  hilo  limefanya    katika  shule  mbali mbali  ndani ya  mkoa  wa Iringa na nje ya  mkoa  wa  Iringa  zimebaini  uwepo  wa  vikwazo  vya  ufaulu kwa  watoto  wa  kike   pindi  wanapokuwa katika  siku  zao  za  hedhi.

Hivyo  kutokana na  changamoto   hiyo  waliona  njia  pekee ya  kumsaidia mtoto wa  kike  kusoma  kwa raha wakati  wote ni kuja na mkakati  wa  kumsaidia  upatikanaji  wa  taulo  za  kike  wakati  wote awapo shule na  njia rafiki  ya kumwezesha  kupata  huduma ya taulo  hizo  bure  ni kuanzishwa  miradi ya ushonaji wa taulo za  kike  ambazo zitakuwa za kufua  .


Mkurugenzi  huyo  alisema  shirika  hilo  na  wadau  mbali mbali kama Malala Fund  na  wengine  waliweza  kujitolea  vyerehani kwa  ajili ya  kuziwezesha   shule  kuanzisha  miradi ya  ushonaji wa taulo  za  kike  katika  shule  ili kuwapatia  bure mabinti  wote  wawapo  shule .

” Kutokana na mkakati  huo  Afya Plus  tumeamua  kutoa  mashine  tano  kwa  kila  shule  kwa  shule  15  za  kuanzia  kati ya  shule 50  zitakazonufaika na mradi huo  ili  kuanza kuzalisha  taulo  za  kike mashuleni  ili  kumwezesha  mtoto  wa  kike  kuwepo  darasani  wakati  wote  wa siku  zake “

Hata   hivyo  alisema  shirika   hilo  linatoa  shukrani kwa serikali ngazi ya   wilaya hadi  Taifa  kwa  kutoa  baraka  za  kuendelea  na mradi  huo mashuleni  na  wao  wanaamini  kupitia  mradi  huo  utasaidia kwa  kiasi kikubwa  kuongeza  wastani wa ufaulu kwa  watoto  wa  kike  wakiwemo  wale  waliokuwa  wakishindwa  kuhudhuria  vipindi  wakati  wa siku  zao .

Kwani  utafiti  uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) na mashirika  mengine   ulionesha  kuwa  watoto  wa  kike  wengi  wanashindwa  kwenda  shule kwa  kipindi  cha kati ya  siku tatu hadi tano  kutokana na  kukosa  uwezo  wa  kifedha wa  kununua taulo  za  kike lakini  pia  kukosekana kwa maji mashuleni .

Kwa  hali  hiyo   wao kama  shirika la  Afya  Plus  waliamua  kuja na mkakati  wa  kuanzisha maabara ya  Hedhi  salama kwa  kutoa  mashine 45  ambazo  kwa  kila  shule itapata mashine  tano na  wameanza na shule  15  kati ya  shule  hizo 50  zilizopo kwa mradi huo  utakaofikia  mabinti  zaidi ya  36600 ndani ya  mkoa wa  Iringa .


Kwa  upande  wake  mwalimu  wa  afya  shule ya  Sekondari  Ipogolo  Iringa Munira  Mabruki  alisema  msaada  huo  uliotolewa na Afya Plus  utakuwa ni  ukombozi  mkubwa kwa  changamoto  za  mtoto  wa  kike  awapo  shule na kuongeza umakini  wa masomo kwa  watoto .

Hivyo  aliomba wadau  wengine  kuendelea  kujitokeza  kumsaidia  mtoto  wa kike  kuondokana na changamoto  za  Hedhi  awapo  shuleni ili  kumfanya  atumia muda  wake  mwingi  kufuatilia masomo .

Mgeni rasmi katika tukio hilo Martha  Luhambano   aliye Muwakilisha Afisa elimu mkoa wa Iringa amesema kuwa vifaa na elimu inayotolewa na shirika la  afya Plus vitasaidia kuondoa changamoto za hedhi  kwa Watoto wakike shuleni na kuokoa afya zao kwa kuwaepusha kupata madhara ya kutumia vifaa ambavyo si salama na kuwataka walimu kuhakikisha vifaa walivyopokea vinatunzwa na vinafanya kazi .