Serikali yaiomba crdb kutoa elimu ya fedha kwa wanufaika wa fidia migodi ya liganga ya nchuchuma njombe

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Wakati vijiji vya Nkomang’ombe na Mundindivilivyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe vikiwa kwenye hatua za mwisho za kuanza kulipa fidia ya zaidi ya bil 11 kutokana na kuridhia kupisha maeneo yao yenye hazina kubwa ya madini, Serikali imetaka tasisi za fedha kwa kushirikiana na maafisa maendeleo kwenda kutoa elimu ya matumizi bora ya fedha na uwekezaji kwa wanufaika ili kuwaepusha na matumizi yasiyofaa ikiwemo ulevi.


Wakazi wa vijiji vya Mundindi na Nkomang’ombe vyenye hazina kubwa ya madini ya chuma na mkaa wa mawe wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu ahadi ya serikali kulipa fidia maeneo yaliyochukuliwa na serikali baada ya kubainika kuwa na madini.

Kiwango kikubwa cha fedha zinazotarajiwa kuliowa kama fidia kwa wananchi walipisha maeneo yao kimewaibua viongozi na watumishi wa umma kuanza maandalizi mapema ya kutoa elimu kwa wananchi ili pindi watakapolipwa fedha hiyo waitumie vizuri ikiwa ni pamoja na kubuni miradi ya kiuchumi badala ya kuongeza wanawake na ulevi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa tawi la benki ya CRDB wilayani Ludewa baadhi ya viongozi wa serikali pamoja watumishi wa umma akiwemo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratus amesema kwakuwa serikali ipo kwenye hatua za mwisho kuanza kulipa fidia kwa wananchi wa Mundindi na Nkomang’ombe waliyopisha miradi ya Liganga Nchuchuma ni vyema taasisi za fedha hususani CRDB kuanza kupita vijiji kutoa elimu kwa wanufaika juu ya matumizi bora fedha hizo.

“Katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya sita ikitarajia kuanza kulipa fidia kwa wananchi waliyopisha migodi ya Liganga na Nchuchuma niwaombe CRDB mshirikiane na maafisa maendeleo wangu kutoa elimu ya fedha kwa wanufaika ili waweze kubuni miradi na kujikita kwenye ujasiriamali,Alisema Sunday Deogratusa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa.

Mbali na masuala ya elimu ya fedha mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Zakarius Kamonga ametumia fursa hiyo kuomba maofisa wa benki kutazama makundi mbalimbali hususani bodaboda na kuyapa mikopo ili waweze kujikimu na kuendesha maisha yao.

“Mimi ni miongoni mwa watu waliodiriki kuvamia hafra za benki hii kwa lengo la kushawishi waweze kuja kufungua tawi ludewa hivyo niwaombe pia kuyatazama makundi ya bodaboda na wajasiriamali wadogo na kuwapa mikopo,Alisema Joseph Kamonga mbunge wa Ludewa.

Mara baada ya kupokea maombi hayo ndipo maofisa kutoka benki hiyo akiwemo meneja biashara wa CRDB Kanda ya nyanda za juu kusini Japhary Katura pamoja na Jenipher Tondi wakaahidi kuyafanyia kazi maombi hayo huku wakisema tayari mchakato wa kuanza kupita kutoa elimu na kuwafungulia akaunti wananchi wa vijiji vitakavyonufaika umeanza kufanyika.

Kuhusu mikopo maofisa hao wamesema benki hiyo ipo tayari kutoa mikopo kwa wajasiriamali,wakulima na kisha kutoa elimu ili shughuli zao ziweze kuleta mapinduzi ya kiuchumi wilayani Ludewa.

“Nikutoe shaka mh mkuu wa wilaya ,Benki itatekeleza haraka iwezekanavyo ushauri na maombi yenu na tuna uzoefu mkubwa na masuala ya ulipaji wa fidia kwasababu tumefanya mahala pengi nchini,Alisema Japhary Katura meneja biashara wa CRDB Kanda ya nyanda za juu kusini.

Kwa upande wake mgeni rasmi Daniel Ngalopela ambaye ni katibu tawala wilaya ya Ludewa  aliyemwakilisha mkuu amesema wakati huduma za kibenki zikiendelea kuimarika ,serikali nayo imeendelea kuboresha huduma nyingine za kijamii ikiwemo afya ,elimu pamoja miundombinu ya barabara lengo likiwa ni kufanya maandalizi ya machimbo hayo.

Ngalopela amesema kusudio la serikali ni kufanya machimbo ya mkaa wa mawe na chuma na kisha kuongeza thamani kwa kuzalisha malighafi katika eneo hilohilo hivyo kuna kila sababu ya benki hiyo kushikamana na serikali kwa lengo la kusaidia wananchi.

“Ni kwamba serikali inampango wa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya madini haya hapahapa ludewa na ndiyo sababu ya kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali hususani barabara,Alisema Daniel Ngalopela katibu tawala Ludewa.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Rose Komba wameishukuru benki hiyo kwa kutambua mahitaji ya usalama wa fedha zao na kisha kufungua tawi Ludewa ambapo wanasema awali walikuwa wakiweka fedha ndani na kuibiwa mara kwa mara na vibaka.