Na Seif Mangwangi, Arusha
WATOTO wadogo wametakiwa kuonyesha ujasiri tangu wakiwa wadogo ili kuwajengea uwezo wa kuweza kutetea haki zao na kuweka wazi vitendo vya kikatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa na watu mbalimbali.
Mtoto Victor Pascal Ntatau mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Maemaki iliko Veta Singida akizungumza kwenye mdahalo kuhusu haki za watoto uliokuwa ukiendeshwa na shirika la Save the Children na LSF katika wiki ya azaki inayoendelea jijini Arusha amesema yeye alijengewa ujasiri tangu akiwa mdogo.
Anasema watu katika kada mbalimbali wameweza kumjengea ujasiri na kumuwezesha kuzungumza katika halaiki ya watu jambo ambalo lilimuwezesha kwenda nchini Denmark kuiwakilisha nchi kwenye Baraza la watoto Duniani.
Victor anasema ukiondoa wazazi wake kumjengea ujasiri katika umri wake mdogo wa miaka 10 aliokuwa nayo sasa, pia waandishi wa habari pamoja na mbunge katika jimbo la singida vimenjengea uwezo mkubwa na ujasiri.
“Kabla sijaenda Denmark kushiriki kwenye kikao cha baraza la watoto duniani, nilijengewa uwezo na watu wengi sana, na kila mmoja aliniambia victor utaweza tu, katika kile kikao tulitoka na maazimio ambayo tuliyawasilisha kwa Marais wa Umoja wa Mataifa,”amesema.
Wakichangia mada katika mdahalo huo, wazazi na wanafunzi wamesema vitendo vya ukatili wa watoto bado vinaendelea nchini jambo ambalo linatakiwa kupingwa vikali kwa kuwajengea ujasiri watoto wadogo ili waweze kuyaibua matukio kama hayo.
Renalda Masawe mkurugenzi wa shirika la Wote sawa, anasema vitendo vya kikatili vimekuwa vikifanywa kwa makundi mbalimbali ikiweo Wafanyakazi wa ndani ambao wamekuwa hawalipwi kiwango kinachotakiwa kulingana na viwango vilivyowekwa na Serikali.
“Pia kuna vijana wadogo wanaajiriwa mtoto chini ya miaka 14., tumeweza kuona watoto wanaagizwa tu kuja mjini kufanyakazi na akifika mjini mzazi anataka, kipato ambacho mtoto anastahili kukipata yeye ndio apewe, na wazazi wamekuwa wakigombana kwa kipato hiki cha mtoto,”anasema.
Hata hivyo anasema watu wamekuwa wakiajiri watoto watoto kutokana na udhaifu wa mtoto husika ambapo anayemuajiri huweza kummudu na kumtendea lolote na hatokuwa na sehemu yoyote ya kwenda kuisemea na wengine wamekuwa wakiwachapa au kuwanyima chakula.
Blandina Nkini anasema Mkoa wa Arusha umefanikiwa kufungua mabaraza ya watoto katika ngazi ya sekondari na yamekuwa yakifanya vizuri sana kwa kuibua vitendo vya kikatili dhidi ya watoto.
Hata hivyo anasema Mkoa ulisahau kufungua mabaraza hayo katika ngazi ya shule ya Msingi na kutokana na kuwepo kwa matukio ya ukatili katika ngazi hiyo, wameshaanza mchakato wa kuanzisha mabaraza ya watoto katika ngazi ya shule ya msingi.