Wakazi arusha kupewa msaada wa kisheria kupitia azaki kuanzia kesho

 Na Zulfa Mfinanga Arusha.

Wiki ya AZAKI inayotarajiwa kuanza kesho Jijini hapa imelenga kutoa msaada wa kisheria kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha kwa lengo la kuleta maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, mratibu wa wiki ya Azaki 2022, Dk Shirley Mushi amesema hatua hiyo inatokana na jitihada zinazofanywa na Asasi hizo kwa kuwafikia wananchi, kufahamu mahitaji yao na kuyapatia ufumbuzi.

Dkt Mushi amesema tangu kuanzishwa kwa wiki ya AZAKI mwaka 2018 matokeo yameonekana ikiwa ni pamoja na ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini pamoja na kuongezeka kwa umoja na mshikamano miongoni mwa wadau.

“Mashirika, taasisi, sekta binafsi, Asasi za kiraia na Serikali, vyuo vikuu na hata mashirika ya kidini ni miongoni mwa washiriki katika wiki ya AZAKI, ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa lengo ni kuhakikisha ushiriki huu unasaidia kisukuma mbele maendeleo ya wananchi na Taifa pia”

Amesema mada zitakazojadiliwa zitagusa Maisha ya binadamu mmoja mmoja ikiwa ni pamoja na mkulima, mama lishe, huku masuala ya utawala bora, uchumi na teknolojia yatajadiliwa pia.

“Pia makundi yaliyoachwa nyuma kwa maana ya wanawake, wazee, walemavu na watoto nayo ni sehemu ya majadiliano yetu, na kuhusu teknolojia tunataka kuiambia jamii kuwa hata teknolojia ndogo inaweza kuwakomboa, siyo lazima iwe teknolojia kubwa, na kuhusu uchumi tunataka kujengeana uwezo ili tutumie fursa zetu tulizonazo kujitegemea na siyo kutegemea wafadhili tu wa nje pekee” alisema Dkt Mushi.

Akifungua wiki ya AZAKI mwezi Agosti mwaka huu Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema Ushirikiano baina ya AZAKI na sekta binafsi utasaidia kutatua changamoto kwa kiasi kikubwa pamoja na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kauli mbiu ya wiki ya AZAKI 2022 ni ‘Maendeleo ya Watu, Habari Fanikiwa za Watu’ .