Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Wahasibu katika Sekta ya Maji wametakiwa kufanyia kazi maeneo yenye changamoto yakiwemo maeneo ya ufungaji wa hesabu za mwisho na mikataba ili kuepusha kujirudia mara kwa mara kwa hoja za kiukaguzi.
Maelekezo hayo yametolewa hivi leo Oktoba 06, 2022 Jijini Mwanza na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Maji, CPA. Ahadi Msangi aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Wahasibu wa Sekta ya Maji.
Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, CPA. Msangi aliwakumbusha wahasibu jukumu lao la msingi la kuweka mifumo ya udhibiti (internal control) ili kupunguza hoja za ukaguzi na uwezekano wa kusababisha hasara kwa Serikali na utendaji usioridhisha
“Katika usimamizi wa fedha yapo maeneo ya kuboresha kutokana na hoja zinazotoka kila mwaka kuna nyingine zinajirudia; natumaini kutokana na kikao hiki mtakuja na maboresho ama maazimio kwenye maeneo ya mahesabu na mikataba ambayo kila mwaka yanajitokeza,” alielekeza.
CPA. Msangi alisema miongoni mwa majukumu makubwa ya wahasibu ni kuhakikisha mali za umma zinatumika kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu, miongozo na ushauri wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali na aliwasisitiza kuhakikisha wanazingatia maelekezo wanayopewa.
“Ikumbukwe kwamba ni wajibu wa Wahasibu kuhakikisha taarifa zinaandaliwa kwa viwango vya kimataifa na kusimamia masuala yote ya mali na fedha za serikali pamoja na kushauri masuala yote yanayohusiana na mambo yahusuyo usimamizi wa fedha,” alielekeza CPA. Msangi kwa niaba ya Katibu Mkuu.
Aidha, aliwakumbusha wahasibu wote wa Sekta ya Maji kuzingatia maadili ya taaluma zao ambayo ni pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na weledi.
Awali akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa kwa kikao hicho, Mwenyekiti wa Wahasibu wa Mamlaka za Maji nchini, CPA. Leonard Chale ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Maji Dodoma alisema lengo la kukutana kwao ni kupata uelekeo wa pamoja kwa wahasibu wote walio chini ya Wizara ya Maji.
“Tumekutana hapa kubadilishana uzoefu, kujengeana uwezo kulingana na hali halisi ya kazi zetu, kujadili changamoto tunazokutana nazo na kupata ufumbuzi wa pamoja,” alisema CPA Chale.
CPA. Chale alibainisha kuwa kikao kazi hicho ni maelekezo ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ambayo aliyatoa kwa watumishi wote kwenye Sekta ya Maji kuhakikisha kila kada inakutana kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja ili kwa maenedeleo ya sekta.
Kikao kazi hicho cha siku mbili kinafanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) maarufu kama Maji House kuanzia tarehe 6 hadi 7 Oktoba, 2022 na kinashirikisha Wahasibu kutoka Wizara ya Maji Makao Makuu, Mamlaka za Maji, Ofisi za Mabonde, Chuo cha Maji, RUWASA na Mfuko wa Maji.