Na Claud Gwandu, Arusha
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limemtunuku Tuzo maalam,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuendeleza, kuimarisha na kuhamasisha utalii nchni
Tuzo hiyo maalum imetolewa jana usiku katika hafla ya tatu ya Utoaji wa Tuzo za kutambua mchango wa wadau wa utalii nchni mwaka 2022, iliyofanyika makao makuu ya TANAPA jijini hapa.
Katika hafla hiyo, iliyoenda sambamba na maadhimisho ya siku ya utalii duniani,jumla ya tuzo 19 zilitolewa kwa makampuni mbalimbali ya utalii yaliyoingiza mapato mengi na kuongoza kwa ubunifu.
Akikabidhi tuzo hiyo maalum ya Rais Samia,kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chana, aliyepokea kwa niaba yake,Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA,Jenerali Mstaafu George Waitara,alisema Rais Samia amestahili tuzo hiyo kwa jitihada zake aliyofanya za kufufua na kuimarisha sekta ya utalii nchini.
“Rais amepambana kuinua sekta hii na sasa tunaona watalii wamefika Bara na Visiwani,sababu ya jitihada na ubunifu wake wa kitengeza filamu ya The Royal Tou wakati hali ya Utalii ilikuwa mbaya, wadau wengi waliathirika baada ya janga la Uviko -19.
Sasa wote tunafuraha wageni wamefurika sababu ya jitihada na ujasiri wa Rais Samia, na anastahili tuzo hii,” alisema.
Alisema kwa hali ilivyo sasa wanaamini ifikapo mwaka 2025/2026 watalii wataongezeka kutoka milioni 1.5 ya sasa, hadi kufikia watalii milioni 5 na kukusanya mapato yatokanayo na utalii Dola za Kimarekani Bilioni 6.
Jenerali Waitara aliwataka wawekezaji zaidi kuwekeza katika sekta ya Utalii nchini kutokana na wingi wa vivutio vilivyopo nchini na kuboteshwa kwa miundo mbinu mbalimbali vinavyorahisisha utoaji wa huduma bora kwa watalii.
Akipokea tuzo ya Rais Samia kwa niaba yake, Waziri Chana, alishukuru TANAPA kwa kutambua mchango na ujasiri wa Rais Samia katika kufufua sekta hiyo muhimu na inayochangia asilimia 17 ya pato la taifa.
Alisema tuzo hiyo na nyingine zimetolewa wakati muafaka kwa sababu kila mwaka Septemba 27 huadhimishwa Sikh ya Utalii Duniani.
“Nawaomba wadau wa utalii tuendelee kuahirikiana na serikali,ili tuweze kufikia lengo la kupata watalii hawa tunatarajia kuwapokea na naamini tutafanikiwa, sababu hali ya watalii kuingia nchini ni nzuri na kila mmoja anafurahia sababu ya jitihada za Rais Samia,”alisisitiza.
Tuzo za TANAPA za kutambua mchango wa wadau wa Utalii zilianza kutolewa mwaka 2019 na Kisha mwaka 2020 lakini hazikutolewa mwaka jana kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mafua(UViKO-19),ulioathiri sana sekta ya Utalii duniani.