Adakwa na tani moja ya bangi

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Polisi mkoani humo imemtia mbaroni mtu mmoja mkulima na mkazi wa kijiji cha Kabulanzwili wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma akituhumiwa kupatikana na madawa ya kulevya aina ya bangi yanayokadiriwa kuwa na uzito wa tani moja.



Kamanda mkoa Kigoma Ramadhani Kingai akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma alimtaja mtu aliyekamatwa kuwa ni Lije Nicholous maarufu kama Madeberi (48) mkulima na mkazi wa kijiji cha Kabulanzwili wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Kamanda kingai alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa na polisi waliokuwa doria akiwa kwenye harakati za kusafirisha madawa hayo ya kulevya kwenda kuuza ambapo haijalezwa mara moja yalikuwa yakipelekwa wapi.

Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa kwa sasa mtuhumiwa huyo anashikiliwa katika kituo kikuu cha polisi mkoa Kigoma sambamba na magunia ya bangi yaliyokamatwa na kwamba upelelezi unaendelea ili kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.

Katika tukio lingine Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa polisi mkoani humo imewatia mbaroni watu watatu kati ya wanne wanaotuhumiwa kutekeleza mpango wa kumbaka msichana mmoja mwanafunzi katika chuo cha waganga kilichopo mkoa Tanga akiwa mwaka wa kwanza ambapo vijana hao walimbaka msichana huyo kwa wakati mmoja.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Ramadhani Kingai akizungumza mjini Kigoma leo asubuhi aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Julius Yelenimo (25), Hemed Miosho (24), Bakari Hassan (21) na mthumiwa wanne ambaye amekimbia jina lake halikuweza kupatikana.

Maelezo ya Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma yanaeleza kuwa watuhumiwa kwa pamoja walimkamata msichana huyo na kumuingiza ndani ambapo walifungulia muziki kwa sauti kubwa ili kufanya sauti ya msichana huyo kuomba msaada isisikike hivyo kutekeleza kitendo chao na baadaye kukimbia hadi walipotiwa mbaroni na polisi.