Kampuni ya obc yahusishwa mgogoro wa loliondo

Kina Mama wa Kimaasai wakiwa wamepiga picha na bango linaloonyesha kutomtaka mwekezaji kampuni ya OBC, picha hii ilipigwa Septemba 15, 2011 katika tamasha la jinsia, kwenye viwanja vya TGNP Jijini Dar es salaam. Mwekezaji OBC amekuwa na mgogoro wa muda mrefu na wakazi wa eneo hilo ambao ni wamaasai jamii ya wafugaji. (Picha ya mtandao)

 Na Mwandishi Wetu,
Loliondo

WANANCHI katika vijiji
vinavyozunguka eneo la pori tengefu la Loliondo wamedai zoezi linalofanywa na
Serikali la kumega ardhi yao kilometa za mraba 1500 linatokana na shinikizo la
kampuni ya utalii ya Ortelo Business Cooperation (OBC) inayowekeza katika eneo
hilo.


Wakizungumza kwa
nyakati tofauti, wananchi hao wamesema tangu mwaka 1992 wamekuwa na mgogoro
mkubwa na kampuni hiyo ya kiarabu ya OBC kutokana na nia ya kampuni hiyo kutaka
kuchukua eneo hilo kw aajili ya shughuli zake za uwindaji.


Kampuni ya Ortelo
Business Cooperation Ltd (OBC), inamilikiwa na familia ya mfalme wa Umoja wa
Falme za Kiarabu (UAE), imekuwa ikiwekeza Loliondo kwa zaidi ya miaka 30 sasa
huku ikiendesha shughuli za uwindaji pamoja na utalii
.


Mwenyekiti wa kijiji
cha Arash, Kiaro Orminis anasema Serikali inachokifanya ni kutaka kuhalalisha
eneo hilo kwa mwekezaji huyo ambaye kwa miaka mingi amekuwa akishindwa kufikia
makubaliano na vijiji vinavyozunguka eneo hilo la uwekezaji na badala yake kumekuwepo
na migogoro isiyoisha.


Onesmo Ole Ngurumwa,
Mkurugenzi wa THRDC na ambaye pia ni mwananchi wa kijiji cha Ololosokwani
anasema awali eneo lote la Loliondo lilijulikana kama pori tengefu la
wanyamapori, lakini lilikuja kubadilishwa na sheria mpya ya wanyamapori
iliyotungwa mwaka 2009 ambayo pia ilifuta sheria ya uhifadhi  wanyamapori ya mwaka 1974.


“Mabadiliko ya sheria
ya Wanyamapori yalibadili hadhi
ya mapori tengefu na kuondoa shughuli zote za kibinadamu kama ilivyokuwa awali. Sheria hii imepiga marufuku
shughuli zote za kibinadamu katika maeneo ya mapori tengefu ambayo kimsingi
yalikuwa yamepachikwa katika ardhi za Vijiji kwa kuwa lengo lake lilikuwa ni
kusimamia rasilimali za wanyamapori na sio milki ya ardhi,”anasema Ole Ngurumwa
na kuongeza:

 “ Bahati mbaya
zoezi hili kwa upande wa Loliondo halikufanyika kama sheria ilivyoagiza, badala
yake kumekuwemo na maneno mengi kuwa bado Loliondo nzima ni pori tengefu 
kinyume na utaratibu wa sasa wa kisheria ambao hauruhusu pori tengefu 
kuchangamana na shughuli za kibadamu,”. 


Hata
hivyo anasema
baada ya miaka ya 1990 makampuni binafsi kushamiri
katika sekta ya  utalii wa uwindaji, kampuni
ya Ortello Business Cooperation Ltd ilipewa eneo lote la Loliondo la Kilometa
za mraba 4000 la vijiji vya Loliondo na Sale.


Anasema baada ya
kampuni hiyo kupewa eneo hilo migogoro mingi ilizuka baina ya kampuni hiyo, wananchi
na watumiaji wengine wa ardhi  ya vijiji
kama makampuni mengine yanayofanya shughuli ya utalii  eneo hilo kabla ya kutungwa kwa sheria mpya
ya wanyamapori ya 2009 iliyoondoa maeneo ya pori tengefu kuwepo kwenye ardhi ya
vijiji.


Kwa upande wake Isaya Ole
Naing’iria anasema baada ya kampuni hiyo ya OBC kushindwa kupokonya ardhi ya
vijiji, ilikubali kukaa meza moja na vijiji vinavyozunguka eneo inalolitumia
kufanyia shughuli zake na kuvilipa vijiji hivyo fedha kama sehemu ya kodi ya
uwekezaji kutokana na matumizi ya eneo hilo.


“Hata hivyo wananchi
tuliamua kuachana na mwekezaji huyu kutokana na mgogoro wa mara kwa mara wa
malisho, alikuwa akizuia mifugo yetu isikaribie eneo la kunyweshea maji lakini
pia eneo la malisho hasa wakati wa ukame na hivyo tukaamua kuachana nae. Miaka
yote hii hakukubali kuondoka aliendelea kutumia eneo hili kwa mabavu huku akisaidiwa
na askari,”anasema.


Mwenyekiti wa Kijiji cha
Ololosokwani Keri Dukunyi anasema wao kama vijiji hawaitaki kampuni ya OBC
lakini inachoonekana ni Serikali kushinikiza mwekezaji huyo aendelee kuwepo
kwenye eneo hilo kwa kuwa anaipatia fedha nyingi.


Anasema pamoja na
kutoomtaka mwekezaji huyo, vijiji vilikuwa vikiendelea kupata pesa kutoka kwenye
kampuni zingine za utalii ambazo zimekuwa zikifuata masharti ya vijiji hivyo hivyo
serikali kupokonya eneo la kilometa za mraba 1500 ni kuwafanya kuwa maskini kwa
kuwa hawatapata tena fedha hizo.


Hata hivyo pamoja na
madai hayo ya wananchi, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa inatenga eneo hilo
kwa ajili ya kulinda mazalia ya Wanyamapori, mapitio na vyanzo vya maji kwa ajili
ya ustawi wa hifadhi kwa manufaa ya Wananchi wenyewe na Taifa kwa Ujumla.


Alama ambayo itatumika kama ukingo wa eneo ambalo ni sehemu ya kilometa 1500 zinazotengwa kwaajili ya uhifadhi

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akizungumza wakati wa kuaga mwili wa askari anayedaiwa kupigwa mshale katika zoezi hilo. Mwili huo wa Koplo Garlus Mwita ulisafirishwa kwenda Mara kwaajili ya Mazishi

Aidha Serikali imekanusha
kuwaondoa wananchi hao kwa lengo la kumpatia mwekezaji yeyote eneo hilo bali
zoezi hilo lina nia ya kuhakikisha usimamizi endelevu wa Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti, Ngorongoro na Pori Tengefu la Loliondo kwa ajili ya kizazi cha sasa
na kijacho.
Mkurugenzi wa OBC Issack Mollel alipotafutwa kuweza kuzungumzia kauli ya wananchi hao kuhusu kudaiwa kujihusisha na mgogoro huo hakuweza kupatikana na hata jitihada za kufika ofisini kwake zilizoko uzunguni Jijini Arusha kwaajili ya kuonana nae, ziligonga mwamba baada ya kukuta lango kuu la kuingilia ofisini kwake kufungwa na hakukuwa na mtu yoyote wa kufungua.