Na Queen Lema,Arusha
Taasisi ya Future STEM Business Leaders kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi
Arusha ( Arusha Technical College ) wameandaa na kutoa mafunzo ya siku nne kwa
wanafunzi wa kidato cha tano na Sita katika Jiji la Arusha kutoka katika shule
Saba zilizopo mkoani hapa
Akifungua mafunzo ya siku 4 kwa wanafunzi hao kaimu Mkurugenzi mtendaji
wa atamizi ya DTBi Dkt Easton Mlyuka alisema kuwa bado kuna mambo hasa ya
teknolojia ambayo yanatakiwa yafanyike ili taifa lizidi kukua kuanzia ngazi za
chini
Alibainisha kuwa katika ustawi wa uchumi wa nchi ya Tanzania kuna
wategemea wataalamu wetu wa ndani na kwa kupitia programu hiyo maalaum ya
sayansi teknolojia na ubunifu itasaidia kuweza kuwapata
“Lengo halisi ni kuona kuwa haya mafunzo hayo yatasaidia sana kupata
kizazi cha watafiti na wabunifu katika nyanja mbali mbali hapa nchini”ndio
maana leo tumewakutanisha wanafunzi hawa
Alisema kuwa mradi huo ulianzia kwenye vituo vya kitaaluma ili kukuza mawazo
na kuyapeleka katika ubunifu na pia kuyabadilisha na kuwa bidhaa na kisha
kuyapeleka ni sokoni na kutumika kwenye jamii.
“Tulianza programu hii na shule 5 kwa mwaka 2019 na tulikuwa na wanafunzi 40
Mpaka sasa tunao wanafunzi 85 na shule 17 pia tulianzia jijini Dar es salaam
lakini sasa tupo Arusha ambapo awali Kwa Arusha Tulianza na shule tano na Sasa
tumeongeza mbili kwahiyo Kwa hapa Arusha tu tunashule Saba zilizopo katika
programu hii “. Alisema Dk Mlyuka.
Alifafanua kuwa pindi unapokuwa na wazo lazima uwe na ubunifu kwa kile unacho
kiona kwenye jamii ili kuweza kupata suluhisho ya jambo hilo, ambapo wazo hilo
lazima liwe na manufaa kwa jamii na linatakiwa liwe na ubora wa ubunifu na
kutoa matokeo chanya ambayo mwishowe litatumika na jamii kisha kuleta faida na
kusaidia kutoa ajira pia ukiwa na wazo lazima uwe na upeo mkubwa wa
kufikilia na uweze kulifanyia kazi kwa haraka.
Dkt Mlyuka alisema kwamba, ili kufanikisha ubunifu na kupata matokeo chanya
kunatakiwa kuwe na ushirikishwaji wa wataalamu mbali mbali ambapo aliwataka
wanafunzi hao kuwa wepesi katika kuomba ushirikiano kwa walimu wao pamoja na
wataalamu walionao
Kwa upande wake Meneja wa Mradi huo Josephine Sepeku, alisema kupitia mradi
huo anaamini mafunzo hayo wataishi nayo kwa muda mrefu na yatatoa matokeo
chanya katika masomo yao na yatapelekea kuwa wabunifu wazuri na wataalamu
wazuri katika nchi.
Alisema madhumuni ya mradi huu hasa ni kwa wanafunzi wa kidato cha tano na
sita na mradi huu wa sayansi ubunifu na biashara utawasaidia sana wanafunzi
hao kuweza kukuza mawazo yao ya kisayansi kuyapeleka zaidi katika
biashara
alibainisha kuwa taifa linaposema
Tanzania ya viwanda ili kuwe na viwanda lazima kuwe na wataalamu wa kutoka
ndani ya nchi na ndiyo maana wameanza kwa kutoa mafunzo ya nadharia ili kuzidi
kuwajengea uwezo toka wakiwa mashuleni.
Naye Kaimu Mkuu wa chuo cha Arusha Technical Dkt. Yusuph Mhando, alisema
kwamba wamekuwa wakitoa mafunzo mbali mbali katika chuo cha ATC na wanafunzi
wamekuwa ni bora zaidi na anategemea mafunzo hayo yatawajenga vyema katika
elimu yao.
“Chuo chetu kimekuwa daraja bora kwa wanafunzi wote wanao pita hapa kwaajili
ya kujifunza mambo mbali mbali hasa katika ufundi, ubunifu wa kisayansi
kwakuwa nyie mmeonyesha dhamira nzuri ya kuwa sehemu ya kuendelea kujifunza
nina imani kubwa sana mtakuwa sehemu ya mafanikio ya kupata wataalamu mbali
mbali katika nchi yetu hasa katika maswala ya uwekezaji wa viwanda”. Alisema
Dkt Muhando.