Na Pamela Mollel, Iringa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa Mafunzo kwa Waandishi wa Habari wa Mitandao ya Kijamii (Bloggers/Youtubers),kutoka mikoa mbalimbali nchini kuhusu Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Jumanne Juni 14,2022 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa Iringa,ambayo yanawakutanisha wanahabari mbali mbali kutoka mitandao ya kijamii nchini.
Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Said Ameir amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa uhamasishaji na ushirikishwaji wa makundi maalum vikiwepo vyombo vya habari katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23,2022
Amesema kuwa waandishi wa habari za mitandao ya kijamii watajengewa uelewa kuhusu changamoto za kuripoti wa sensa kwa vyombo vya habari, wajibu wa vyombo vya habari katika kufanikisha sensa ya watu na makazi 2022, vyanzo vikuu vya uripoti kwenye sensa ya watu na makazi.
Katika mafunzo hayo ya siku mbili waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii watajengewa uwezo/uelewa kuhusu Sensa na Sheria ya Takwimu,umuhimu wa Sensa ya watu na makazi na maandalizi yake,madodoso ya sensa na maudhui yake, maeneo ya kuhesabia watu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,Matumizi ya Teknolojia katika sensa ya watu na makazi kutoka kwenye makaratasi hadi kwenye Kishikwambi.
Aidha Mtaalam wa Idadi ya watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Hellen Siriwa, akiwasilisha mada ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na Maandalizi yake, amesema Waandishi wa Habari wana wajibu wa kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuhesabiwa kwani Sensa ni zoezi la Kitaifa ambalo utekelezaji wake unahusisha makundi na taasisi zote nchini ambazo zina nafasi ya kusaidia utekelezaji wa Sensa.
Aidha Wanahabari wana wajibu wa kuelimisha na kuhamasisha Sensa katika namna yoyote ile ili mradi ujumbe ufike na hatimaye kila mwananchi aone umuhimu wa kuhesabiwa.
Kushirikiana na Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya kwa mawazo na ushauri wenye lengo la kujenga, kupunguza gharama, na wenye tija ambao hatimaye utapelekea mafanikio mazuri ya zoezi hili la kitaifa.
Kutumia majukwaa na shughuli za kila siku kusambaza ujumbe wa Sensa, kuweka ujumbe wa Sensa katika machapisho, tovuti na mitandao ya Kijamii kuelimisha jamii