Wananchi loliondo walalamika ardhi yao kuvamiwa

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella akishiriki zoezi la kuchimba shimo kwaajili ya kuwekea alama (Beacoans) katika eneo la Kilometa za Mraba 1500 Loliondo

 

Na Mwandishi Wetu,
Loliondo

Kufuatia zoezi linaloendelea
la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la pori tengefu la Loliondo (Loliondo
Game Controlled Area), Wananchi wanazounguka eneo hilo wameshangazwa na hatua hiyo
ya Serikali na kudai kuwa zoezi hilo linafanywa bila ridhaa yao.


Wakizungumza kwa nyakati
tofauti, wananchi hao wamesema eneo hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1500
limepunguzwa kutoka tarafa ya Loliondo na Sale lililokuwa na ukubwa wa kilometa
za mraba 4000 kabla ya kupunguzwa na serikali na kwamba kinachofanywa ni kuwapokonya
wananchi ardhi yao.


Hata hivyo wamesema kwa
kuwa wananchi wenyewe hawajakubaliana na zoezi hilo bado kuna meza ya majadiliano
inaweza kufanyika kati ya wananchi wanaozunguka eneo hilo na Serikali ili kufikia
muafaka.


“Sisi wananchi hatujakubaliana
na hii hatua ya serikali ya kugawa eneo letu, wanasema wanapunguza eneo la
kilometa za mraba 1500 na kutubakizia 2500, kwa makubaliano gani? kama wanataka
eneo letu ni vyema wakaja tuzungumze,”anasema Melau ole Olobikoki.


Melau anasema eneo hilo
wamekuwa wakilimiliki kihalali kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa ardhi ya mwaka
1923 na mabadiliko ya sheria ya Ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 ambayo ilitamka
wazi kuwa vijiji vitapewa hatimiliki ya Ardhi na wao wanazo hati hizo.


“Kwa kweli tunashangazwa
na hatua ya Serikali kulivamia na kuanza kulipunguza eneo letu  tunalomiliki kihalali bila ridhaa yetu na
mbaya zaidi inafanya hivyo huku ikitambua inavunja sheria inayozisimamia yenyewe,”anasema.


Kwa mujibu wa Mkuu wa
Mkoa wa Arusha, John Mongella mpango wa Serikali ni kupunguza eneo la kilometa za
mraba 1500 kulifanya kuwa hifadhi pekee na kwamba hakuna mwananchi hata mmoja
ambaye ataondolewa katika maeneo hayo.


Mongella amesema eneo
la Loliondo ni ekolojia muhimu ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti lakini pia ndio
mazalia ya wanyamapori wengi hivyo Serikali inataka kulitunza eneo hilo
kwaajili ya faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Aidha Mkuu huyo Mkoa
amesema kuwa tafiti mbalimbali zinasema eneo hilo ndio chanzo cha maji
yanayotumika na wakazi wa tarafa ya Loliondo lakini pia maji hayo hutiririka
kuelekea mto Mara unaotumiwa na wanyama katika hifadhi ya Serengeti na Masai
Mara nchini Kenya.