Dc mboneko atoa maagizo kwa sungusungu shinyanga

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko amewataka  viongozi wa jeshi la sungusungu Wilaya hiyo kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoanzishwa na serikali kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza leo kwenye mkutano wa kusimika  viongozi wa sungusungu ambao wamechaguliwa katika kijiji cha Kolandoto Wilayani Shinyanga, kwenye  viwanja vya shule ya Msingi Kolandoto ambapo  DC Mboneko ameeleza kuwa wana wajibu wa kukabiliana na vitendo vya ubadhirifu wa fedha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi.

Mkuu wa Wilaya Mboneko amewataka viongozi kufanyakazi wa weredi, kusimamia  haki kwa wananchi na kuhakikisha wanafuata kanuni za jeshi la sungusungu ili kuimarisha usalama.

“Viongozi mliochaguliwa mkatende haki kila mmoja wenu mkasome hizo kanuni vizuri na mzisimamie vizuri zisilete mgongano mkatekeleze vizuri, muda umeisha twende kwenye kazi, kazi ziendelee kama anavyosema mheshimiwa Rais, serikali inaleta fedha kwenye kata zetu kwa ajili ya kutatua kero za wananchi lakini wengine wanakula hela za serikali sasa hawa wanaokula hela za serikali muwalete kwenye mkondo wetu wa sheria na muwafikishe kwenye jeshi la sungusungu”.

” Mwananchi ukiona jambo haliko sawa peleka kwenye ngazi husika mimi niendelee kuwaomba sana tuendelee kushirikiana, kushikamana Shinyanga ni yetu sote kunapokuwa na amani na utulivu mambo yanaenda vizuri kwahiyo tuendelee kumuomba mwenyezi Mungu sehemu ambako hakujatulia pawe na utulivu tuhakikishe Kolandoto inaendelea kuwa salama na kata zingine zote  mimi kamanda wenu mkuu niko vizuri na nitaendelea kuwapa ushirikiano muda wote”.

Mheshimiwa Mboneko  amewaomba wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali huku akiwasisitiza kujenga utaratibu wa kutoa taarifa za viongozi wanaoenda kinyume na matakwa ya serikali kwa kufanya ubadhirifu wa fedha za miradi ili kuweza kujinufaisha.

Bi Jasinta Mboneko pamoja na mambo mengine amewakumbusha wazazi na walezi  kulea watoto katika maadili mema kwa kufuata misingi ya Mungu ambapo amewaomba wazazi hao kusimamia maendeleo ya watoto shuleni huku akiwaagiza viongozi wa jeshi la sungusungu kusimamia suala hilo ili watoto wote waweze kupata haki yao ya elimu.

Aidha pia Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga amewashukuru wananchi kwa kutoa ushirikiano katika zoezi la anwani za makazi huku akiwaomba kutoa ushirikiano kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Mwaka huu 2022.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi waliochaguliwa  leo wameahidi kushirikiana na serikali katika kukabiliana na vitendo vya ubadhirifu ili kuleta maendeleo kwenye jamii na kwamba wamesema hawatakubali kuona ubadhirifu wowote unafanyika.

Katika mkutano huo wamechaguliwa viongozi katika nafasi mbalimbali ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti msaidizi wa jeshi la sungusungu kijiji cha Kolandoto Ngamila Nyahilu, Kamanda mkuu wa jeshi hilo Athuman Geneya, Kamanda msaidizi wa jeshi hilo Manoni Bundala pamoja na wajumbe 30 wa sungusungu kijiji hicho cha Kolandoto. 

Mkutano huo pia umehudhuria na viongozi mbalimbali  wa serikali pamoja na viongozi wa sungusungu Wilaya ya Shinyanga mjini ambao wamefuatana na viongozi wa sungusungu matawi 18 ya Manispaa ya Shinyanga pamoja na matawi 3 ya jirani Kishapu ambapo zoezi hilo limefanyika vizuri.