Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iraghe |
Na Marunda Oko Kitaru, Moshi
Kutokana na mafanikio ya uzinduzi wa filamu ya Royal Tours katika Jiji la Arusha iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranqhe ameamua kuanzisha Tamasha la Kimataifa la Utalii wa Michezo la Arusha ili kuunga mkono juhudi za Rais.
Kwa ushirikiano na Chama cha Ngumi za Ndondi Duniani (WABA) Dira ya Mstahiki Meya Maximilian Iranqhe ni kutumia faida na fursa nyingi iwezekanavyo ambazo Rais Samia Suluhu Hassan amesaidia kutengeneza katika kukuza utalii.
“Tutawaalika wanamichezo kutoka Marekani, Ulaya, Asia na nchi nyingine za Afrika ambazo huleta watalii wengi kutembelea Tanzania kama vile Afrika Kusini, Misri na Morocco kushiriki katika tamasha hili. Lengo ni kulitangaza Jiji la Arusha kama kitovu cha utalii katika Afrika Mashariki’ alisema kwa majigambo Meya Maximilian Iranqhe ambaye anaongoza pengine jiji safi zaidi nchini Tanzania.
Tamasha la Kimataifa la Utalii wa Michezo la Arusha litashirikisha michezo ya ngumi za kulipwa, soka, mpira wa kikapu na mbio za marathon ambazo zitashirikisha wanamichezo toka Tanzania na wanamichezo wa kigeni.
Katika mchezo wa ndondi kwa mfano, mikanda mitatu ya awali ya ubingwa wa Afrika na ubingwa wa dunia kwa wanaume na wanawake imesha tengenezwa nchini Pakistani tayari kwa tamasha hilo.
Michezo mingine Zaidi itaongezwa kwenye tamasha hilo kila mwaka kutokana na umaarufu wake miongoni mwa wadau wa utalii na linatazamiwa kuwa mojawapo ya matamasha maarufu zaidi ya Utalii wa Michezo barani Afrika kusini mwa Sahara. Tarehe maalumu ya tamasha hilo imepangwa kufanyika siku ya Nane Nane (Agosti 8, 2022)
Juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii zinapaswa kuungwa mkono na viongozi wa serikali na jamii yote ya Watanzania na Meya Maximilian Iranqhe anakuwa wa kwanza, shukrani kwa maono yake makubwa ya kuifanya Arusha kuwa Geneva na Dubai ya Afrika katika masuala ya utalii na biashara.