Baadhi ya wadau wa kilimo cha Mbogamboga, Matunda na Maua walimsikiliza Karibu Mkuu |
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara akizungumza na wadau na wawekezaji wa kilimo cha Mbogamboga,Matunda na Maua pichani |
Mkurugenzi wa ukanda wa ukuzaji wa kilimo kusini (SAGCOT) Geogrey Kirenga wa kwanza kulia na Mkurugenzi wa TAHA Jackline Mkindi walimsikiliza Katibu Mkuu Professa Godius Kahyarara |
Baadhi ya wadau na wawekezaji wa sekta ya kilimo cha Mbogamboga, Matunda na Maua wakiwa katika picha ya Pamoja na Katibu Mkuu |
*Yajipanga kumaliza kero za wawekezaji
*TRA, NEMC, OSHA watakiwa kujitathmini
Na Seif Mangwangi, Arusha
SERIKALI kupitia kituo cha uwekezaji nchini (TIC), imesema imejipanga kumaliza kero za muda mrefu ambazo zimekuwa zikidumaza sekta ya uwekezaji nchini na kusababisha baadhi ya wawekezaji kusitisha shughuli zao na wengine kushindwa kuwekeza baada ya kutoridhishwa na mazingira yaliyokuwepo.
Akizungumza leo Aprili 29, 2022 wakati wa kufungua kikao kilichokutanisha wadau wa sekta ya kilimo cha mbogamboga, matunda na maua nchini (Horticulture), Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda, na Biashara Professa Godius Kahyarara amesema sekta hiyo ni miongoni mwa sekta muhimu nchini na imekuwa ikiingizia Serikali mapato mengi kupitia wawekezaji na hivyo kero zake zinapaswa kutatuliwa haraka.
Amesema endapo kero mbalimbali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa ndani ya sekta hiyo zitatatuliwa, watanzania wengi watapata ajira kwa kuwa wawekezaji wengi wamekuwa wakikimbilia sekta hiyo kuwekeza kutokana na changamoto nyingi za kidunia zinazotokana na mabadiliko ya kidunia na kwamba hivi karibuni Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan imesaini mikataba mikubwa ya uwekezaji katika sekta ya kilimo katika nchi za Dubai na Marekani.
Prf Kahyarara amesema katika kikao hicho pia zimealikwa taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Mapato nchini TRA, OSHA na NEMC, kwa lengo na wao kusikiliza kero ambazo wawekezaji wamekuwa wakikutana nazo wakati wanapofanya operesheni zao na kuzifanyiakazi.
Amesema Mheshimiwa Rais alishatoa maagizo kwa Mamlaka ya Mapato nchini pamoja na taasisi kama za OSHA, NEMC na idara ya kazi kutokutumia nguvu kudai kodi za Serikali na kuondoa urasimu kwenye utoaji wa vibali hivyo Wizara yake imeamua kuendelea kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha wawekezaji wanalindwa na hawadaiwi kodi kwa nguvu.
“Hizi mamlaka zimekuwa zikilalamikiwa sana na wawekezaji, lakini Mheshimiwa Rais alishatoa maagizo, tumewaita hapa ili wasikilize kero ambazo wawekezaji wanakumbana nazo, na sisi tutazipokea na kuzifanyia kazi, hii sekta ni sekta muhimu sana na ikisimamiwa vizuri inaweza kutoa mapato mengi na kuipiku hata sekta ya utalii,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini Dkt Maduhu Kazi amesema kituo cha uwekezaji kimeamua kuwaita wadau wa sekta ya kilimo cha mbogamboga, matunda na maua ili kusikiliza kero wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za kila siku na kufanyia kazi mawazo ambayo watayatoa.
“Lengo letu ni kuhakikisha wawezekaji wanaongezeka mara dufu nchini, hivi sasa maeneo mengi yamefunguka, tuna masoko hadi ufaransa kwa hiyo ni lazima tuhakikishe kero zilizopo zinatatuliwa haraka sana kabla mambo hayajaharibika,”amesema.
Amesema kituo cha uwekezaji kimeendelea kupunguza baadhi ya kero zilizokuwepo ikiwemo utoaji wa vibali vya kazi kwa wafanyakazi wageni na kuongeza idadi ya wageni wanaopaswa kuajiriwa kwa kampuni moja, kupunguza kodi ya uwekezaji na hivi sasa inaendelea kukamilisha mfumo wa matumizi ya huduma kielekroniki ili kuwarahisishia wawekezaji popote walipo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya kilimo cha mbogamboga, matunda na maua nchini (TAHA), Jackline Mkindi ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuonyesha nia ya kuondoa kero mbalimbali ambazo wawekezaji wamekuwa wakikabiliana nazo katika sekta hiyo ikiwemo kutafuta masoko ya kimataifa.
Amesema kero zilizobakia ni pamoja na kukosekana kwa usafiri wa ndege inayotoka moja kwa moja nchini hadi ulaya kupeleka mazao hayo na badala yake wamekuwa wakitumia Nairobi nchini Kenya jambo ambalo limekuwa likiwasababishia hasara kubwa kutokana na wingi za mizigo iliyopo katika kiwanja hicho na kupelekea baadhi ya bidhaa kuharibika kwa kukaa muda mrefu uwanjani.
“Juzi baadhi ya bidhaa zetu ziliharibikia kiwanja cha ndege cha Jomo Kenyata Nairobi baada ya kukaa muda mrefu kusubiri usafiri wa ndege na kukosa, tunaomba Serikali inunue ndege yake lakini pia iboreshe bandari yetu, kwa mizigo inayopitia baharini tumekuwa tukisafirishia kupitia bandari ya Mombasa jambo ambalo sio sawa kabisa,”anasema.
Ametaja kero nyingine kuwa ni pamoja na magari yanayosafirisha bidhaa kutoka shambani kusimamishwa vituo vingi na muda mrefu na askari wa usalama barabarani kwaajili ya ukaguzi jambo ambalo limekuwa likiwasababishia wawekezaji hasara kwa kuwa magari hayo huhifadhi bidhaa kwenye jokofu na hivyo hulazimika kutozima gari kwa muda wote ambao hufanyiwa ukaguzi.