Serikali yatakiwa kuwashirikisha wataalam wa kilimo kufufua zao la shayiri

 

 

Na Claud Gwandu, Arusha

  

SERIKALI imetakiwa kuwashirikisha kikamilifu  wataalam wa kilimo hasa watafiti katika
kuendeleza kilimo cha Shayiri ambacho ni zao muhimu la biashara.

 

Shayiri ni zao linalofanana na ngano ambalo
hutumika kama malighafi ya kuzalisha kinywaji cha bia ambacho hutumiwa na
watanzania wengi.

 

Mratibu wa zao la Shayiri nchini, Salome Munisi
anasema kuwa kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa Shayiri nchini kinatisha na
kwamba hatua za makusudi lazima zichukuliwe kuliokoa zao hilo.

 

 

Salome ambaye pia ni mtafiti katika Kituo cha
Utafiti wa Kilimo TARI Selian kilichopo jijini Arusha, aliwaambia wanahabari
walioshiriki mafunzo ya sayansi na utafiti yaliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH) iliyofanyika jijini hapa hivi karibuni kuwa  mahitaji ya zao hilo nchini ni makubwa lakini
uzalishaji ni mdogo.

 

“ Inasikitisha kuona zao ambalo lilikuwa tegemeo
la wakulima katika baadhi ya mikoa nchini sasa limesahaulika na Shayiri karibu
yote inabidi iagizwe nje jambo ambalo halina tija kwa uchumi wa nchi na
wakulima,” anasisitiza Mratibu huyo .

 

Akitoa takwimu, mtafiti huyo anaeleza kuwa
asilimia 80 ya mahitaji ya shayiri nchini inaagizwa kutoka Kenya na Afrika
Kusini anaeleza kuwa,hali hiyo haina tija wala manufaa kwa nchi na wakulima wa
zao hilo.

 

Alitoa sababu ya kushuka kwa uzalishaji wa zao
hilo pamoja na ngano kuwa ni kukosekana kwa mipango endelevu ya kusaidia
wakulima ikiwa ni pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika.

 

Hata hivyo,Serikali imekuwa ikisisitiza kuwasaidia
wakulima wa ngano na shayiri na kutengenezea mazingira mazuri wakulima wa
shayiri na ngano ili wapate masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

 

Takwimu zinaonyesha kuwa uzalishaji wa shayiri
nchini kwa mwaka 2020 ulikuwa tani 20 392 
 ambao ni ongezeko kidogo
ulikinganisha na miaka ilittopita.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa
Mataifa (FAO),uzalishaji wa shayiri ni mdogo nchini pamoja na kwamba Tanzania
ni miongoni mwa mataifa 86 duniani yenye mazingira bora ya kuzalisha zao hilo.

 

Zao hilo nchini linalimwa kwa wingi katika mikoa
ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambako wakulima huvuna wastani wa kilo 500
kwa eka ingawa wataalam wa kilimo wanasema kuwa uwezekano wa mavuno kufikia
hadi kilo 1000 kwa eka,iwapo hatua madhubuti zitachukuliwa, upo.