Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema kuwa litaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni mkakati wa kuendelea kupunguza ajali huku likielezea kwa sasa matukio ya ajali hizo yamepungua kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza jana baada ya kushuhudia wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio jijini Dar es Salaam wakitoa hukumu mbalimbali kwa madereva ambao wamevunja sheria za Usalama Barabarani kupitia ‘Mahakama ya Watoto’ Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa amesema elimu inayoendelea kutolewa inasaida kupungua matukio ya ajali barabarani,hivyo wataendelea kuitoa mara kwa mara.
Kamanda Mutafungwa ameongeza katika kutoa elimu hiyo ya usalama barabarani kwa ajili ya kuwajengea uelewa wa kuepuka ajali kwa kufuata sheria za Usalama barabarani Jeshi hilo limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa Shirika la Amend ambao wamekuja na ubunifu wa kuanzisha Makamma ya Watoto ambayo lengo lake ni kuendelea kutoa elimu hiyo ili kufika kwa jamii kubwa ya Watanzania.
“Ninachoweza kukieleza, ni kwamba matukio ya ajali za barabarani yamepungua kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na huko nyuma.Kuna sababu nyingi ambazo zimesababisha kupungua kwa ajali za barabarani lakini miongoni mwa sababu ni elimu inayoendelea kutolewa sambamba na kuwahamiza madereva wa magari,bajaji na bodaboda kuheshimu sheria.
Pia elimu hii inatolewa kwa watembea kwa migumuu na njia mbalimbali zinatumika kufikisha elimu hiyo,”amesema Kamanda Mutafungwa na kuongeza kwamba Mahakama ya Watoto imekuwa njia nyingine ya kuifikisha elimu hiyo na matarajio yao ni kuona inaendelea katika maeneo mengi zaidi kwani kwa mujibu wa Shirika la Amend ambao ndio wameratibu programu ya mahakama hiyo wanaeleza inafanyika katika shule nane za msingi ambazo ni za Serikali.
Akiizungumzia zaidi programu ya Mahakama ya Watoto iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia wanafunzi wa Shule za msingi,Kamanda Mutafungwa amesema itasaidia kufika elimu hiyo kwa wananchi wengi zaidi na kwa haraka zaidi.
“Kupitia Mahakama ya Watoto tumeona Watoto wetu( wanafunzi) ambavyo wanafahamu sheria za usalama barabarani na hata wakati wanaoendesha kesi dhidi ya madereva waliovunja sheria mbalimbali za barabarani unaona wanavyosikiliza na kutoa hukumu.
“Madereva wanakiri kuvunja sheria mbele ya wanafunzi, wanatoa ahadi ya kutorudia makosa na watakuwa mabalozi kwa kuwaambia madereva wengine waheshimu sheria,hakika Mahakama hii inafikisha elimu katika Mazingira rafiki na sisi Kikosi cha usalama barabarani tunaifurahia na kuwapongeza Amend kwa ubunifu huu,”amesema Kamanda Mutafungwa.
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Amend Simon Kalolo amesema wao kama wadau wa usalama barabarani wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama barabarani kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani.
“Katika kuendelea kutoa elimu tumeamua kuja na programu ya Mahakama ya Watoto na lengo kuhakikisha tunashirikiana na wenzetu Polisi kufikisha elimu hii.Programu ya Mahakama ya Watoto imezaa matunda na kwetu tunaona faraja namna wanafunzi walivyokuwa na uelewa mkubwa wa kusikiliza kesi za madereva wavunjifu wa sheria na hukumu zinavyotolewa.Madereva wanaulizwa maswali ya msingi na wanafunzi hawa,”amesema Kalolo.
Kwa upande wa wanafunzi walioko kwenye programu ya kutoa elimu ya Usalama Barabarani kupitia Mahakama ya Watoto wamesema wanalishukuru Jeshi la Polisi na Shirika la Amend kwa kuandaa programu hiyo na kuombe iwapo kuna uwezekano isambae kwenye shule zote nchini wakiamini itakwenda kusaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo nyingi zinazotokana na watumiaji wa barabara kutofuatwa sheria