Jeshi lawarejesha kambini vijana 853 wa jkt iliowafukuza 2021

 MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Nchini, (CDF), Jenerali Venance Mabeyo ametoa msamaha kwa Vijana  853 waliofukuzwa katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa, (JKT)  April 12, 2021 kutokana na makosa ya kinidhamu.


Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Machi 05, 2022 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema kuwa CDF Mabeyo  ameamuru Vijana hao wote warejeshwe katika kambi za JKT tayari kwa kuanza mafunzo yao mara moja.


Amesema kuwa Mnamo April 12,2021  Jumla ya Vijana wa Kitanzania 854 ambao walikuwa wanaendeea na mafunzo ya kujitolea kwenye kambi za  JKT, walifukuzwa na kuondolewa kambini na kurejeshwa majumbani mwao kutokana na makosa ya kinidhamu .


“JWTZ imepokea na ina taarifa Kijana mmoja kati ya wale Vijana 854 amefariki na walio hai ni Vijana 853,” imesema sehemj ya taarifa hiyo. 


Luteni Kanali Ilonda ameeleza kuwa Jenerali  Mabeyo ametoa msamaha kwa vijana hao baada ya JWTZ kufanya uchunguzi wa kina na utafiti na kujiridhisha  kuwa vitendo hivyo vya ukiukwaji wa taratibu za kinidhamu walivyifanya ni kwasababu ya utoto.


“Wengi wao walifanya hivyo kwa kutojitambua, kurubuniwa na wengine walifanya kwa kufuata mkumbo,” imesema taarifa hiyo ya Luteni Kanali Ilonda


Aidha, amedai kuwa kuna baadhi ya Watanzania walioshiriki kuwarubuni Vijana hao na kutoa wito wa kutofanya vitendo hivyo


“Tuache Vijana wapate mafunzo yao ya stadi za maisha ili waje kulitumikia Taifa lao kwa moyo mmoja,” amesisitiza Luteni Kanali  Ilonda. 


Awali April 17, 2021 CDF Mabeyo aliwafukuza vijana hao wakati wa  hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mjini Dodoma.


“Aprili 8,  2021 vijana wetu wa JKT wapatao 854 walianzisha mgomo,  kukataa kufanya kazi maeneo mengine  na kufanya maandamano kwenda Ikulu kwa madai ya kutaka kumuona rais ili wadai kuandikishwa jeshini kama walivyoahidiwa na aliyekuwa rais wa Tanzania,  John Magufuli.”

“Vijana hao ni kati ya vijana 2400 walioahidiwa kuandikishwa jeshini na walifanya uamuzi huo baada ya jeshi kuamua kuwapunguza katika kazi ya ujenzi wa Ikulu Chamwino baada ya kazi kupungua ili waende kufanya kazi katika maeneo mengine lakini wao wakapinga kwa madai wangekosa kuandikishwa jeshini, ” alisema Mabeyo.

Alibainisha kuwa jeshi halikuwa na lengo hilo na limelazimika kusitisha mikataba yao kwa kuwa kosa walilolifanya ni sawa na uasi na hauvumiliki.

Alieleza kuwa pamoja na  kufanya uchunguzi  wa kwa nini walifanya hivyo,  jeshi limeamua kutafakari upya mpango wa kuchukua vijana wa kujitolea kwa ajili ya kujiunga na JKT.