Meya wa jiji la Arusha Maximilian Iraghe akipanda mti katika shule ya msingi Mirongoine wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti elfu10 |
Na Seif Mangwangi,Arusha
Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iraghe jana Machi4, 2022 amezindua rasmi kampeni ya kupanda miti 10,000 katika kata mbili za Olmot na Muriet ndani ya Jiji la Arusha. kampeni hiyo inendeshwa na Taasisi ya Foundation for Environment and protection in Tanzania (FEPT),
Akizungumza katika shule ya msingi Mirongoine iliyopo katika kata ya Olmot Jiji la Arusha, katika hafla fupi ya zoezi hilo, Meya Iraghe amesema kukosekana kwa miti kumekuwa kukisababisha madhara mengi kubwa ikiwa ni kukosa majira sahihi ya mvua.
Amesema tukio la kupanda miti elfu10 lililofanywa na shirika la FEPT linapaswa kuungwa mkono na wadau wote kwa kuwa lina malengo mazuri ya kubadilisha mandhari ya Jiji la Arusha na kusaidia kutokomeza tatizo la ukosefu wa mvua.
Meya Iraghe ameutaka uongozi wa shirika la FEPT kubadilisha aina ya miti inayopanda na kuanza kupanda pia miti ya matunda ili waweze pia kupata na matunda baada ya miti hiyo kukua.
“Tunawapongeza sana FEPT kwa ubunifu huu, miti ni uhai, miti inaleta kivuli kizuri na pia hewa ya oksijeni tunaipata vizuri kupitia miti, lakini nawaomba mbadilishe aina ya miti mnayoipanda angalieni uwezekano wa kupanda miti ya matunda,”amesema.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa FEPT Peter Mhamgama amesema kwa msaada wa shirika la maendeleo la watu wa Canada, wameweza kuendesha zoezi hilo kwa mwaka wa pili sasa.
Ametaja changamoto anazokabiliana nazo katika mradi huo kuwa ni pamoja na baadhi ya wakazi katika maeneo ambayo wanapanda miti kung’oa miti hiyo na kuitupa bila sababu, kuingiza mifugo na kukosekana kwa maji ya kunyeshea.
” Mheshimiwa mgeni rasmi katika zoezi hili la kupanda miti tumekutana na changamoto kadha ikiwemo uhitaji mkubwa wa maji kwenye maeneo tunayopanda hususani mashuleni, tunakuomba unapokuwa kwenye baraza la madiwani muangalie pia suala hili,”amesema.
Amesema katika zoezi hilo pia wameshirikiana na wakala wa Misitu Tanzania (TFS), pamoja na kampuni ya bia TBL, na kwamba mbali ya kupanda mashuleni pia watagawa miti mingine kwa wakazi wanaozunguka maeneo ya shule.