Ucheleweshwaji haki chanzo cha mauaji, vitendo vya kikatili

Na Joctan Mnyefu

Kufuatia kukithiri kwa mikasa ya mauaji na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake , Serikali imeshauriwa kuanza kutoa elimu ya haki za binaadam kuanzia ngazi ya familia, shule za msingi hadi chuo kikuu.

Katibu mkuu wa Baraza la maaskofu Tanzania TEC Dkt Charles Kitima  amewataka wasomi nchini kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na matukio hayo ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii juu ya masuala ya haki za binadamu kuanzia ngazi ya chini kabisa ambayo ni familia.

Katika mdahalo ulifanyika kwa njia ya Mtandao ukikutanisha wasomi na viongozi wa imani ukiangazia hali ya haki za wanawake na mauaji  ya kikatili nchini chini ya Ufadhili wa shirika la Freedom House, Dkt Kitima amesema mauaji ,vipigo na unyanyasaji wa kila aina unaofanywa kwa mwanamke ni kinyume cha mpango wa mungu.

Amesema wakati umefika wakupinga vikali vitendo vya mauaji ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa jamii pamoja na  kulifanya somo la haki za binadamu kufundishwa katika ngazi zote za elimu.

“Tunapaswa kuonyesha kwamba kuua mwanamke ama kufanya ukatili wa aina yeyote kunakiuka na kuvunja haki za binadamu na ili kutokomeza vitendo hivi tunapaswa kuanza kutoa elimu kwa jamii zetu ambapo tunapaswa kuingiza somo la haki za binadamu katika mitaala mashuleni hadi vyuoni,”alisema Dr Charles Kitima katibu wa baraza la maaskofu Tanzania TEC.

Kuhusu maandiko matakatifu kiongozi huyo wa kiimani anasema Biblia nayo imeweka bayana juu ya nafasi ya mwanamke na mwanaume kuwa ni sawa na kwamba yeyote atakaejaribu kufanya ukatili kwa mwanamke ni ukiukwaji mkubwa wa misingi ya kiimani.

“Mwanamke na mwanaume wote ni sawa hivyo kusiwepo na utamaduni wa kufanya jambo kwa kutoa kipaumbele kwa mwanaume na kumuweka nyuma mwanamke ,alisema Dr Charles Kitima 

Aidha Dkt Kitima amesema ili kuweka usawa baina ya mwanamke na mwanaume jamii zinapaswa kutilia mkazo haki za binadamu na kuwa na hofu ya mungu kwasababu kitendo cha kuondoa nafasi ya mwenyezi mungu katika maisha yetu ya kila siku ndiyo sababu ya kuibuka kwa kasi kwa matukio yanayoendelea hapa nchi na mataifa mengine ulimwenguni.

“Juzi tumeona mtu kauwawa kanisani wakati hapo ndipo injili inapotolewa ,hali hii ni matokeo ya kutokuwa na hofu ya mwenyezi mungu,Alisema katibu mkuu wa baraza la maaskofu Tanzania TEC Daktari Charles Kitima .

Kwa upande wake mjumbe kutoka Bakwata Taifa, Shekh Swed Twaib Swed amesema tatizo la mauaji linasababishwa na mambo matatu ikiwemo kuvunjika kwa maadili, umaskini pamoja na ucheleweshwaji wa haki ambao umekuwa ukifanywa kupitia vyombo vya serikali vya kutolea maamuzi.

Amesema Qurani ni miongozi kwa vitabu vya Mungu ambavyo vimetoa haki sawa kwa wote hivyo endapo wafu watafuata miongozo iliyopo matukio hayo yatakoma.

” Mimi nashauri elimu kutolewa kwa vijana wetu kuanzia ngazi ya familia, lakini pia vyombo vya kimaamuzi vitoe haki kwa wakati, unakuta mtu anafuatilia haki yake mahakamani mpaka akachoka, mwisho anaamua kujiua,”Anasema.

Katika hatua nyingine Kamishna wa tume ya haki za binaadam na utawala bora, Dkt.Fatma Halfan amezungumzia suala la sheria linavyotambua na kuthamini haki ya kuishi na usawa pamoja na hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na shirika ili kukomesha matukio hayo ambapo amesema katika katiba ya Tanzania Ibara ya 12 na 13 zinatambua usawa wa binadamu na usawa katika sheria ambapo ibara ya 14 yakatiba inaonyesha ni jinsi gani kila mtu anahaki ya kuishi.

Kuhusu jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na tume ya haki za binadamu ni pamoja na kuanzisha klabu zaidi ya 250 kote nchini ambazo zimekabidhiwa jukumu la kutoa elimu ya haki za binadamu katika jamii za kitanzania.

“Katiba ya Tanzania inatambua kuwa Kila mtu anahaki ya kuishi hivyo tunapaswa kusimama imara na kuongeza nguvu katika kupinga mauaji na unyanyasaji unaoendelea dhidi ya mwanamke,”Alisema Dkt.Fatma Halfan.

Awali akiweka bayana sababu za kukithiri kwa matukio ya ukatili dhini ya mwanamke mkurugenzi wa asisi ya Women Promotion Center Tanzania(WPC) Matha Jerome anasema ni pamoja kuwepo kwa mifumo dume katika jamii zetu,Umaskini wa kifikra na kipato,Ukimya,Matumizi ya dawa za kulevya na Ulevi wa pombe kupindukia,Visasi,Migogoro ya ndoa na ardhi hivyo tunapaswa kuanza kukabiliana na mambo haya kwa kutoa elimu kwa wananchi  ili kunusuru maisha ya mwanamke ambayo yako hatarini.

Tatizo lingine ambalo limetajwa kuwa chanzo cha ukatili dhidi ya mwanamke mkurugenzi huyo anasema ni kutotilia mkazo suala la malezi na makuzi ya mtoto na kutoa rai kwa wazazi kuanza kulipa kipaumbele suala hilo.

Akitoa ushauri hatua za kuchukua ili kuanza kudhibiti ukatili Matha Jerome anasema ni vizuri kila mmoja kuanza kulaani na kukemea vitendo vinavyotekelezwa ndani na nje ya ndoa huku pia ushuri ukitolewa kuundwa kamati zitakazopewa jukumu la kufuatilia haki za kikatiba pamoja kufatilia malezi na makuzi ya mtoto ili kupata kizazi kitakachokuwa na maadili na kuzingatia misingi ya katiba yetu.

” Matukio yote haya yanakuja kwasababu ya nguvu kubwa lililopewa kundi moja ambalo ni mwanaume dhidi ya kundi jingine na pindi yanatokea jamii inaona ni sawa tu na kwamba tuna haya ya kufanya mabadiliko ya mifumo tuliyozoea kuishi,Alisema mkurugenzi wa asisi ya Women Promotion Center Tanzania(WPC) Matha Jerome “