Serikali yajidhatiti kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

Meneja wa Mpango wa  Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipeumbele, Dk. George Kabona akizungumza kuhusu kilele cha maadhimisho ya wiki ya magonjwa hayo yatakayofanyika siku ya Jumapili viwanja vya Nyerere Square Dodoma. Wengine ni maafisa wa vitengo mbalimbali kwenye mpango huo.

* Yaweka mikakati kabambe kuyatokomeza

*Ummy mgeni rasmi siku ya kilele jumapili

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

 

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

 

Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni pamoja na usubi, kichocho, minyoo ya tumbo, trakoma/vikope, matende na mabusha.

 

Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Taifa wa Kuratibu Magonjwa hayo Wizara ya Afya, Dk. George Kabona alisema jana kuwa kilele cha maadhimisho hayo yaliyoanza tarehe 24 mwezi huu ni Jumapili tarehe 30 ambayo imetengwa kimataifa kuadhimisha magonjwa hayo.

 

Alisema maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila maka yatafanyika kwenye viwanja vya Nyerere Sqwea mkoani hapa na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali.

 

Alilisema Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyoathiriwa na magonjwa hayo na imekuwa ikitekeleza mpango wa kuyatokomeza hivyo kila mwaka hutenga wiki ya kuadhimisha magonjwa hayo.

 

Alisema lengo la siku hiyo ni kujikumbusha kwamba nchi inawajibu wa kutokomeza magonjwa hayo na kusherehekea mafanikio ambayo yamepatikana katika kuyadhibiti.

 

 “Tunaangalia mafanikio kiasi gani tumepata na kujaribu kuondoa changamoto zilizopo kwa pamoja ili tuweze kufikia malengo kutokomeza magonjwa haya ifikapo mwaka 2030 ili yaondoke kabisa kwenye jami yetu,” alsiema

 

Alisema kuna magonjwa mengi nchini ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele lakini kuna matano ambayo yameathiri kwa sehemu kubwa ambayo kwa miaka 10 serikali imekuwa ikipambana nayo.

 

Alisema magonjwa hayo yako sehemu kubwa hapa nchini na yameathiri watanzania wengi na kichocho kimeonekana kuathiri zaidi watu wengi.

 

Alisema udhibiti wa magonjwa hayo ulianza miaka mingi iliyopita lakini mpango wa taifa wa kuyadhibiti kwa pamoja ulianza mwaka 2009 ambapo magonjwa hayo yaliunganishwa pamoja ili yadhibitiwe pamoja kwasababu yote  yanafanana kwa kuathiri na madhara yake yanaonekana baada ya miaka mingi.

 

“Madhara yake si kiafya tu yanasababisha unyanyapaa kwa jamii na katika mifumo ya kutolea afya hayapewi kipaumbele kiasi kwamba mtu akipata magonjwa haya akienda hospitali si rahisi kupewa huduma,” alisema

Dk. Kabona alisema kupitia mpango huo ulioko Wizara ya Afya, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuhakikisha inahamasisha watu wayatambue na mifumo ya afya iimarishe huduma zake katika vituo vya kutoa huduma.

 

Alisema serikali imekuwa ikitoa elimu kupitia njia mbalimbali ili iweze kujikinga na magonjwa hayo ili watanzania wasipate madhara hayo ambayo huwa yanatokea taratibu.