Watakiwa kupanda miti kukabili ukame

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Katibu wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Agnes Bashemu amewataka Wanachama wa Chama hicho pamoja na  Wananchi wote kwa ujumla kupanda miti kwenye makazi yao,kama hatua mojawapo ya kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia Nchi.

Ameyasema hayo wakati wa zoezi la kupanda miti katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho kuelekea kilele chake Februari 05,Mwaka huu ambapo  chama kitatimiza Miaka 45 tangu kuzaliwa kwake.

Katibu huyo pamoja na mambo mengine amewaomba Wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye Sensa ya Watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Mwaka huu.

“Tunataka kila mwanachama wa CCM apamde mti nyumbani kwake tunataka baada ya Miaka mitano au kumi tule matunda kwa kila kiongozi nyumbani kwake miti ni bure”.

Katika Maadhimisho hayo Chama cha Mapinduzi CCM kimeshiriki shughuli ya upandaji miti katika shule ya msingi Bugoyi A pamoja na Bugoyi B ambapo Walimu wakuu wa shule hizo Elisiana Kimaso mkuu wa shule ya msingi Bugoyi B pamoja na Alex Juma mkuu wa shule ya msingi Bugoyi A  wamesema wataisimamia na kuitunza miti hiyo.

Kwa upande wao wanafunzi wa shule za Msingi Bugoyi A pamoja na Bugoyi B  wamekishukuru chama hicho kwa kupanda miti katika shule hizo ambapo wamesema miti hiyo itawasaidia kupata matunda pamoja na kupendezesha mandhari  ya shule hiyo.

Akizungumza na Misalaba Blog katibu mwenezi wa chama cha mapinduzi CCM kata ya Ndembezi Juliana Busuluga amesema wamepanda miti zaidi ya mia mbili (200)  katika shule hizo.

Diwani wa kata hiyo ya Ndembezi  Victor Thobias Mmanywa baada ya kukamilika zoezi la upandaji miti amezungumza na wananchi ambapo amewaomba kuendeleza amani na ushirikiano uliyopo ili kuendelea kupata maendeleo chanya katika kata hiyo.

Diwani Mmanywa amewahakikishia wakazi wa kata hiyo kuwa ataendelea kuisimamia miradi yote inayoletwa na serikali kwa ajili ya manufaa ya wananchi na kwamba atasimamia suala la ulinzi na usalama ambapo amesema hatokubali kuona vibaka, wezi au uhalifu wowote ule unafanyika katika kata hiyo ambapo amesema kwa sasa hali ya usalama ni shwari.

Mmanywa amewasisitiza wananchi wa kata hiyo kuwa mabalozi wazuri wa kulinda amani ambapo amewaahidi kuendelea kuzitatua changamoto mbalimbali ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya kata hiyo.

Diwani huyo ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani kwa kutoa Milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Mazinge iliyopo kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Aidha diwani Mmanywa amewaomba wananchi wa kata hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali zinazotolewa na viongozi mbalimbali pamoja na juhudi za viongozi wa chama katika ngazi zote kata Wilaya na Mkoa ili kuinua uchumi wa Taifa.

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya wazazi Mkoa wa Tabora Bandora Salum Mirambo akizungumza katika maadhimisho hayo amewaomba wananchi kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali waliopo madarakani kwa lengo la kuhakikisha kila kiongozi anawajibika katika nafasi yake.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia hivi karibuni alichukua fomu ya kugombea kiti cha spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanazania kupitia chama cha mapinduzi CCM Stephen Julius  Masele akiwa katika maadhimisho ya sikukuu ya miaka 45 tangu kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi CCM katika kata ya Ndembezi ametoa shukurani kwa wananchi huku akiwaomba wanachama wa chama hicho kuendelea kushirikiana katika shida na raha.

“Nitumie nafasi hii kusema ahsanteni sana kwa sala na dua zenu ambazo mlikuwa mkiniombea wakati nikiwa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nataka niwaambie kwamba hii ni mbegu ambayo mliipanda ninyi safari yangu ya siasa ilianzia hapa Ndembezi”.

“Niwakumbushe wana CCM wenzangu tuendelee kushirikiana, tuendelee kupendana niwatie moyo tuendelee kushirikiana  kwa sababu hii ni familia kubwa ya wana CCM ni familia kubwa ya wanashinyanga”amesema Masele.