Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi pamoja na Kamishna mteule William Mwakilema wakiteta jambo wakati wakisaini hati za makabidhiano ya ofisi |
Wakisaini hati za makabidhiano ya ofisi |
Na Seif Mangwangi,Arusha
Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi amewataka wafanyakazi wa TANAPA kuendeleza umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya shirika.
Alitoa wito huo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kwa Kamishna wa Uhifadhi mpya William Mwakilema. Alisema “Mafanikio yaliyofikiwa kwa upande wa TANAPA yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kuimarisha mshikamano.”
Alielekeza TANAPA kuongeza bidii katika kuyatekeleza majukumu ya msingi ambayo ni kuendeleza uhifadhi na utalii. Alitahadharisha kuwepo kwa dalili za ujangili katika hifadhi zetu na kusisitiza kuzilinda maliasili hizi kwa nguvu zote.
Kuhusu utalii, alisisitiza kuongeza bidii ili kuwavutia watalii wa ndani na nje. Ili kufikia lengo hili ni lazima kuboresha miundombinu, kutoa huduma bora kwa watalii na kuendelea kuvitangaza vivutio vyetu.