Wanafunzi wa kike elimu ya juu waonywa matumizi mabaya ya mitandao

 

Mwandishi wetu, Arusha

 

Wanafunzi wa kike wanaosoma elimu ya juu nchini, wametakiwa kuwa na matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii na kuacha kujihusisha na kusambaza taarifa zisizo Sahihi zinazokiuka sheria na maadili.

Wakili Leopord Mosha  wa Mtandao wa watetezi wa haki za Binaadamu (THRDC)alitoa wito huo, katika mafunzo ya usalama,ulinzi na sheria za mitandao ya kijamii nchini, kwa wanafunzi wa kike wa elimu juu wanaosoma vyuo vikuu vya Tumaini Makumira, Taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru na chuo Cha mtakatifu Agostino tawi la Arusha.

Akizungumza katika mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya  mradi wa  boresha habari unaofadhiliwa na shirika la  internews  kwa ushirikiano na shirika la misaada la marekani(USAID) Alisema mitandao ina faida kubwa ikitumiwa vizuri.

Mafunzo hayo ambayo yaliendeshwa kwa njia ya zoom, Kwa kuandaliwa  na taasisi ya elimu ya uraia na msaada wa kisheria(CILAO) kwa kushirikisha taasisi ya msaada wa habari kwa jamii za asili za wafugaji, wawindaji na waokota matunda(MAIPAC) na shirika la ustawi wa wanawake na watoto(WOSWELS) yalishirikisha pia wanahabari nchini.

Mosha alisema  ukitumia kinyume cha sheria mitandao  ya kijamii unaweza kujikuta katika mgogoro na hivyo kufikia hadi hatua ya kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“mjuwe tuna sheria na makosa ya mtandao ya mwaka 2015, tuna sheria ya Takwimu, tunasheria huduma za habari ya mwaka 2016,lakini pia kuna kanuni zamaudhui mitandano lazima tujuwe pia Kuna Sheria za kimataifa”alisema

Mkuu wa Kitengo Cha TEHAMA wa Mtandao wa mashirika ya wafugaji,Wawindaji na waokota matunda(PINGOs Forums)Elie Chansa akitoa mada juu ya ulinzi na usalama katika mitandao, aliwataka wanafunzi wa kike kuhakikisha wanakuwa na usalama wa vifaa vyao na usiri.

Alisema kama una akaunti yako ya Email, Twiter,Instragram na nyingine hakikisha unakuwa na Nywira(neno ya siri) ambayo sio rahisi mtu kujua na kuingia kwenye akaunti yako.

“sheria inakataza kumiliki simu ambayo haina nywira na hii inalinda faragha za mtumiaji lakini pia mtu ambaye hausiki wawezi kutumia na kusambaza taarifa za uongo ama uzushi kwa simu yako.”alisema Chansa

“wanafunzi wa kike mmekuwa wahanga wakubwa wa mitandao ya kijamii, sasa lazima mbadilike na msiwe wanyonge, mitando hii ni fursa kujiendeleza kielimu, kujikwamua na umasikini,kutoa taarifa za ukatili lakini kupata fursa za kiuchumi”alisema

Mkurugenzi wa taasisi ya elimu ya uraia na msaada wa kisheria(CILAO) Odero Charles Odero alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike juu ya matumizi salama ya mitandao.

Alisema wanafunzi wamekuwa wahanga wa kufanyiwa ukatili katika mitandao hivyo Sasa muhimu kubadilika

 Mkurugenzi wa Taasisi ya msaada wa habari kwa jamii za asili za wafugaji, wawindaji na waokota matunda(MAIPAC) Mussa Juma alisema Kupitia Mradi huo wanafunzi wa kike watapata mafunzo ya sheria za Mitandao na masuala ya usalama na Ulinzi.

Alisema baada ya mafunzo wanatarajiwa wanafunzi waliopata mafunzo katika mradi huo kuwa mabalozi katika vyuo kuhimiza matumizi sahihi za Mitandao lakini pia kutumia mitandao Kwa faida.

Alisema wanahabari wakiwepo wanawake pia wamepata fursa ya mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo juu ya sheria za Mitandao na masuala ya usalama na Ulinzi wanapotumia mitandao katika kazi zao.

Mkurugenzi wa Shirika la ustawi wa wanawake na watoto(WOSWELS) Mary Mushi alisema wasichana wasiwe wanyonge kwenye matumizi ya mitandao na waitumie kutoa taarifa wakifanyiwa ukatili ikiwepo wa kingono.