Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mwenyekiti wa mtaa wa Miti mirefu kata ya mjini Manispaa ya Shinyanga Nassor Mokhe amewataka waendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu Bodaboda wa mtaa huo kutoa taarifa za uhalibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi mtaani hapo.
Wito huo umetolewa leo wakati wa zoezi la upandaji miti ambalo limefanyika katika mtaa huo ikiwa ni mwendelezo wa kampeini ya serikali ya uhifadhi wa mazingira ambapo pia amewataka bodaboda hao kuzingatia usafi katika vituo vyao vya kazi.
“Niwaombe tuendelee kushirikiana pili mtusaidie kubaini wahalifu kama yumo mhalifu tupeni taarifa tumuondoe kwenye kijiwe tumkabidhi kwenye vyombo vya sheria leo tumeandaa mazingira ya upandaji wa miti sasa mtusaidie kwenye usafi kila kijiwe cha bodaboda tuwe na chombo cha kuhifadhia takataka wale wanao kojoa kojoa pembezoni mwa miti hii tunayoipanda mkamateni faini yake ni Shilingi Elfu hamsini kwahiyo naomba tushirikiane kwa hilo hata kwenye uchafuzi wa mazingira kwa namna yoyote ile ukimuona mtu anachafua mazingira mkamate”.
Wakizungumza baadhi ya Bodaboda hao ambao wameshiriki zoezi hilo wamesema wataendelea kutoa ushirikiano katika kuwakamata wachafuzi wa mazingira na kwamba miti waliyoipanda itasaidia kuondoa hali ya ukame katika mkoa wa Shinyanga.
Kwa upande wake Afisa maliasili Manispaa ya Shinyanga mhifadhi Ezra Manjerenga amewahukuru bodaboda hao kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki shughuli hiyo ya upandaji wa miti ambapo amesema lengo la serikali ni kuhakikisha kila Halmashauri inapanda miti Milioni moja na laki tano.
“Tunalo lengo la kitaifa la kila Halmashauri kupanda miti Milioni moja na laki tano na leo hii tumegusa eneo la lengo letu kwa kupanda miti 261 hamasa inaenda mpaka kwenye kaya kwa kusisitiza kila kaya wapande miti miwili ya kivuli na miti mitatu ya matunda miti tunagawa bure lakini shule za msingi na sekondari wote watapanda miti kwahiyo mimi niwapongeze sana bodaboda ambao leo mmejitolea mmeacha shughuli zenu na kukubali wito wa mwenyekiti wa mtaa ambaye leo ametukutanisha kwa pamoja”
Zoezi la Uandaji Miti katika Mtaa wa Miti mirefu limewashirikisha viongozi mbalimbali wa serikali kuanzia ngazi ya Mtaa hadi Wilaya pamoja na bodaboda ambapo jumla ya Miti 261 imepandwa kwa siku ya leo.