WATU tisa waliokuwa wakisafiri na gari ya kusafirisha magazeti aina ya hiace lenye namba za usajili T 249 DWT wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa .
Mashuhuda wa ajali hiyo wamelieleza Matukio Daima Media ajali hiyo imetokea Leo asubuhi na kuwa gari hilo lilikuwa mwendo mkali na baada ya kufika eneo hilo dereva lilimshinda kukata Kona na kugonga mti .
“Gari hii iliyokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Jijini Mbeya, ilikuwa mwendo kasi kabla ya kupoteza uelekeo na kugonga mti”
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, Dk Iddy Omary amethibitisha kupokea maiti tisa zinazoendelea kutambuliwa.
“Tumepokea maiti tisa katika hospitali yetu, zinazoendelea kutambuliwa,” alisema.
Kuhusu majeruhi taarifa zinaonesha walikimbizwa katika Hospitali Ilula, wilayani Kilolo wanakoendelea kupata matibabu.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa
ACP Allan Bukumbi alisema ajali hiyo imetokea katika kijiji cha cha Mahenge Wilayani Kilolo Mkoani Iringa majira ya saa 10 alfajiri.
Kamanda Bukumbi amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambapo gari hilo lilimshinda dereva kwenye kona na kupinduka.
Hata hivyo Kamanda Bukumbi ametoa Rai Kwa madereva kuwa makini barabarani na kuzingatia sheria za usalama barabarani.