Na Seif Mangwangi, Karatu
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na wakala wa barabara nchini (TANROADS), wameanza mradi wa majaribio wa kufunga Kamera za barabarani katika maeneo ya mkoa wa Pwani na Morogoro pamoja na kusanifu barabara mpya kwa michoro ya kisasa ili kuzuia ajali za mara kwa mara.
Hayo yameelezwa Novemba 27,2021 na Kaimu Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), Mhandisi Kashinde Mussa katika mahojiano wakati wa kufunga maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani iliyofanyika eneo la mlima Rhotia ilipotokea ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent mwaka 2017.
Kaimu Mkurugenzi usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Kashinde Mussa wa kwanza aliyevaa kofia ya blue pamoja na Meneja Usalama na Mazingira wa TANROADS Zafarani Madayi aliyevaa kofia nyeusi wakizungumza na Wandishi wa Habari |
Kwa upande wake , Meneja Usalama na Mazingira wa wakala wa barabara nchini(TANROADS), Zafarani Madayi, amesema baada ya kuona mafanikio kwenye mradi wa Kamera za barabarani kuzuia mwendo kasi kwa mikoa ya Pwani na Morogoro hivi sasa wako kwenye mpango wa kuweka Kamera katika barabara zote nchini lakini pia kuhakiki na kuboresha alama zote za barabarani ili kuepusha ajali.
Aidha, Zafarani amesema katika maonyesho ya wiki nzima yaliyokuwa yakifanyika katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Arusha wadau mbalimbali wameweza kupata elimu ya shughuli za TANROADS katika banda la wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kujifunza kazi ambazo zinafanywa na wizara hiyo.
Amesema wamepokea agizo la Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamisi Chilo ya kushirikiana kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya alama za barabarani na kupunguza ajali na kwamba TANROADS imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kila wakati.
Awali akifunga maonyesho hayo katika eneo la Rhotia ambalo ajali iliyoua wanafunzi wa shule ya msingi Lucky Vincent mwaka 2017, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi , amewataka wadau mbalimbali wa barabara kushiriki kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara ili kupunguza ajali.
“Ndugu zangu vifo vinapangwa na Mungu lakini ajali hazipangwi na Mungu, Nawaombeni kila mmoja atumie nafasi yake kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara, Mheshimiwa Rais Samia ameshatoa maagizo na mimi naendelea kusisitiza kila mmoja afanye matumizi sahihi ya barabara,” amesema.
Amewataka Mabalozi wa usalama barabarani kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani kutoa elimu kwa madereva bodaboda ili kuepusha ajali zonazo sababishwa na uendeshaji mbovu usiozingatia matumizi ya alama za barabarani.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha usalama barabarani SSP Wilbroad Mtafungwa amewataka wadau wa barabara kutafakari vifo vya wanafunzi 30 na walimu2 wa shule ya msingi Lucky Vincent na kuchukua hatua za kudhibiti ajali za barabarani.
“Leo hii wanafunzi hawa hatunao, wamepoteza ndoto walizokuwa nazo na za wazazi wao kwa sababu tu ya dereva mmoja asiyependa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, Nawaombeni sana tutafakari hili,” amesema.
Mei 6, 2017 ndoto za wanafunzi 30 na walimu 2 pamoja na dereva 1 wa shule ya msingi ya Lucky Vincent ya Jijini Arusha zilikatizwa ghafla katika ajali ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda hifadhini, ambapo walipofika katika eneo la Rhotia kwenye mteremko mkali, dereva huyo aliyekuwa katika mwendo wa kasi bila kujali usalama wa wanafunzi alobeba aliserereka na kutumbukia mtaroni.
SSP Wilbroad Mtafungwa akizungumza katika hafla ya kufunga wiki ya nenda kwa usalama barabarani |
Wakuu wa vikosi vya usalama barabarani nchini wakiwa katika picha ya pamoja |