Zanzibar kinara matukio ya kunajisi watoto wadogo , # kilimanjaro inaongoza tanzania bara kwa matukio 6

IGP Simon Siro 

   Na Seif Mangwangi, Arusha

MATUKIO ya kunajisi watoto wadogo yameelezwa kuendelea kuongezeka
nchini licha ya jeshi la Polisi kuendelea kukabiliana na watuhumiwa wa matukio
hayo kwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani na baadhi yao kuhukumiwa vifungo.


Kwa mujibu wa tovuti ya taifa ya takwimu( NBS), kwa mwaka
2019/2020 vitendo vya kunajisi watoto wadogo vimeongezeka kwa matukio 23 ambapo
mwaka 2020 jeshi la polisi limeweza kupokea matukio 52 kutoka matukio 29
yaliyoripotiwa mwaka 2019.


Kwa mujibu wa jeshi la Polisi, Zanzibar ndio inayoongoza kwa
vitendo vya kunajisi watoto wadogo ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Disemba
2020 jeshi hilo lilipokea matukio 46 kwa Zanzibar na matukio 6 kwa Tanzania
bara.


Mkoa wa Mjini Magharibi ndio unaoongoza kwa matukio 28,
ukifuatiwa na Kaskazini Pemba9, Kaskazini Unguja matukio7, na kusini unguja2
huku Tanzania bara Mkoa wa Kilimanjaro ukiongoza kwa matukio 3 ukifuatiwa na
mikoa ya Iringa1, Rukwa 1na Songwe1.


Takwimu hizo pia zinaonyesha katika kipindi cha Januari hadi
Desemba 2020 jumla ya makosa 11,001 yaliripotiwa ikilinganishwa na makosa
12,223 kwa mwaka 2019.

“Huu ni upungufu wa makosa 1,222 sawa na asilimia 10.0.
Makosa yenye ongezeko kubwa la idadi ni Kunajisi (23), Kutupa watoto (5) na
Usafirishaji haramu binadamu (1). Aidha, makosa yaliyopungua sana kiidadi ni
Kubaka (574), Mauaji (394) na Kulawiti (278),”ilisema taarifa hiyo.

Takwimu hizo zinajumuisha makosa ya kibinaadam ya kubaka,
kulawiti, wizi wa watoto, kutupa watoto, kunajisi na usafirishaji haramu wa
binaadamu.

Aidha akizungumza bungeni hivi karibuni, Naibu Waziri wa
Afya Manaidi Ali Khamisi alinukuliwa akisema 
kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu, watoto 6168 walifanyiwa ukatili
wa kijinsia na kati yao 3524walibakwa. Pia alisema wanafunzi 1887 walipata
ujauzito katika kipindi hicho hicho.