Na Seif Mangwangi, Arusha
Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza wakala wa barabara nchini kutengeneza michoro ya watembea kwa miguu na waendesha baiskeli katika barabara mpya zitakazojengwa.
Akizungumza kwenye banda la wizara ya ujenzi na uchukuzi, Rais amesema ujenzi mpya wa barabara unapaswa kuwa na mfumo huo ili kuepusha ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikipoteza uhai wa watanzania wengi.
Pia ameipongeza TANROADS, kwa hatua ya kuongeza mfumo wa alama kwa wenye ulemavu ambao ni wenye ulemavu wa macho, walemavu wa viungo na albino.
Akitoa taarifa ya utendaji ya wakala wa barabara nchini, Mtendaji Mkuu wa TANRODS Injinia Rogatus Mativila amesema TANRODS imekuwa ukitoa elimu ya mara kwa mara kwa watumiaji wa barabara ili kuhakikisha hali ya usalama wa barabara inakuwa bora.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Arusha waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo, Rais Samia ameliagiza jeshi la Polisi nchini kuongeza jitihada za kupunguza ajali.
Amewataka askari wa usalama barabarani kujenga urafiki na raia tofauti na sasa askari wamekuwa wakionekana kama maadui dhidi ya raia jambo ambalo limekuwa likisababisha ajali hususani za bodaboda.
” Kumekuwa na mtindo wa askari wa barabarani kuonekana maadui dhidi ya madereva wa pikipiki, madereva hawa wakiwaona askari wanatafuta njia ya kukimbilia na matokeo yake ni kusababisha ajali, naomba hii tabia ikomeshwe,” aliagiza Rais Samia.
Pia Rais Samia ametoa pongezi kwa baraza la usalama barabarani kwa jitihada zake za kuhakikisha linapunguza ajali za barabarani lakini amelitaka kuongeza jitihada zaidi kukomesha kabisa ajali hizo.
Amemtaka Katibu mtendaji wa Baraza hilo SSP Wilbroad Mtafungwa kubuni njia za kujipatia kipato zaidi ili kuendesha kwa ufanisi baraza hilo na kukataa maombi ya baraza ya kutumia nusu ya fedha zinazokusanywa kwa makosa barabarani katika shughuli zake.
Awali Katibu wa Baraza la usalama barabarani SSP Wilbroad Mtafungwa alisema baraza hilo limekuwa likikabiliwa na ukata wa fedha jambo ambalo limekuwa likikwamisha malengo ya baraza ambayo imekuwa ikijiwekea.