Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya |
Katibu Mkuu Tucta Said Wamba |
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthon Mtaka |
Na Rhoda Simba, Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthon Mtaka amelitaka shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA) kutokuwa na migongano,migawanyiko, na migogoro katika vyama kwani watakosa kauli ya pamoja ya kutetea maslahi ya wanachama wao.
Amesema vyama vya wafanyakazi vina mchango mkubwa kwenye matokeo yanayoonekana hasa kwenye kupanda madaraja,uboreshwaji wa maslahi ya wafanyakazi na makundi mengine ya ajira katika siku za hivi karibuni yameonekana kupata muafaka.
Ameyasema hayo leo Novemba 11 jijini hapa wakati akifungua mkutano mkuu wa saba wa kuchagua viongozi watakaohudumu kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025.
“Nyinyi ni vyama vya wafanyakazi uchaguzi una mambo mengi lakini kwenye mwamvuli huo wa mambo mengi lazima mjitambue mkiingia kwenye hiyo migongano mgawanyiko na migogoro mtakosa kauli ya kuisema serikali kwasababu kama nyinyi wenyewe mnapalangana mnafitishiana mnasemeana mambo mabaya hamtafika,
“Lazima muwe na mshikamano kama nyinyi wenyewe siyo taswira hamtafika Wanachama mnatakiwa muhubiri haki umoja ndani ya vyama vyenu mnao umoja mkikaribisha mambo ya ovyo kwaajili ya uchaguzi wa siku moja mtapotea ,
“Niwaombe uchaguzi wa kesho kazi ya siku moja isiwakosanishe we omba kura tu, mtachafuana lakini mwisho wa siku lazima kiongozi apatikane ogopeni teknolojia msijitoe kwenye maisha ya kuwa viongozi kwajili ya mambo ya ovyo maana leo mtajibizana camera zitahifadhi mwisho wa siku unaanza kusambazwa mitandaoni”amesema Mtaka .
Amesema maana ya kutafuta kiongozi ni kutafuta mtu ambae anaweza kukaa na kutetea wanachama wake na kuzungumzia masilahi,na changamoto za wanachama.
Awali akisoma risala kwa kwa mgeni rasmi Kaimu Katibu Mkuu TUCTA Said Wamba amesema Mkutano huu ni wa saba unachagua viongozi utakaoongoza mpaka 2025.
Amesema kama shirikisho wanafanyia kazi na kusimamia katiba na kutetea vijana kama kauli mbiu inavyo ashiria na kupigania haki ya vijana kupata ajira ya elimu na ujasiriamali.
Wamba amesema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya waajiri kuwazuia wafanyakazi kutojiunga na vyama hivyo kitu ambacho si haki na ni kumnyima uhuru mfanyakazi hata hivyo shirikisho hilo lina wajibu wa kusimamia Haki, wajibu na umuhimu wa mshikamano na kudumisha uhusiano mwema katika kazi na kutetea ajira.
“Takwimu za kila mwaka zinazotolewa na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali zinabainisha kuonekana kwa ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira nchini na hasa kwa vijana.
Takwimu zinaonesha idadi ya ajira inaonesha imezidiwa na idadi ya vijana wanaohitaji.
“Tunashukuru kwasababu vijana wanajiongeza wanafanya ujasiriamali ingawa bado hatuna jinsi ya kuwawezesha mipango yote ya serikali imeonesha mipango mbali mbali, shirikisho linatambua kuwa watu wote hawawezi kupata kazi Serikali “
Kwa upande wake Rais wa shirikisho hilo Tumaini Nyamhokya amesema msimamo wao ni kuendelea kutetea wafanyakazi na kulinda mali za shirikisho nakuwaongezea thamani wafanyakazi.
Nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo ni; Rais, Makamu wa Rais,Katibu,Naibu Katibu mweka Hazina ,Wadhamini.
Wengine ni Mwenyekiti kamati ya wanawake, Makamu mwenyekiti wanawake, pamoja na kamati ya wanawake.
Mkutano huo wa uchaguzi umebebwa na kauli mbiu “isemayo kazi ajira na maendeleo ya wafanyakazi”