Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Kuelekea maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama Barabarani Wakazi wa mkoa wa Shinyanga wameliomba jeshi la polisi kitengo cha usalama Barabarani kutoa elimu sahihi kwa madereva wa vyombo vya moto hasa pikipiki zinazobeba abiria, kuhusu umuhimu wa kuheshimu alama za Barabarani ikiwemo vivuko.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti wakazi wa Manispaa ya Shinyanga ambao wamewalalamikia watumia vyombo vya moto hasa pikipiki za abiria maarufu bodaboda kutozingatia sheria za usalama Barabarani ikiwemo vivuko na kuendesha kwa mwendo kasi.
Samweli Athanas Kitija ni mmoja wa waendesha pikipiki za abiria maarufu Bodaboda amewaomba waendesha bodaboda wenzake kuwa makini, kuheshimu, na kuzingatia sheria za usalama Barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
“Niwaombe bodaboda wenzangu tuwe na uangalifu na umakini mkubwa sana kwa sababu ajali zimedhidi kwetu tunasikia bodaboda ameanguka au amegongwa kwa sababu ya kutokuwa makini tunapofata sheria za barabarani ajali zinakuwa zinapungua na kingine dereva wengine wa bodaboda wanakuwa wanakunywa pombe anaingia barabarani akiwa amelewa hawezi kuwa makini hususa anapokuwa anaendesha chombo chake cha moto”.
Mkuu wa usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Mrakibu wa Polisi Malege Emanuel Kilakala ameendelea kuwataka watumiaji wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama Barabarani ikiwemo kuheshimu vivuko.
“Madereva turudi katika kuheshimu watumiaji wengine wa barabara tuheshimu alama, michoro, vivuko vya watembea kwa miguu tusianze kuonyesha sasa ule udereva wa kushindana kingine madereva watii sheria bila shuruti”.
Maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama Barabarani kitaifa Mwaka huu yatafanyika Mkoani Arusha kuanzia Novemba 11,na kilele chake kitakuwa Novemba 20,ambapo kauli mbiu yake inasema “Jali Maisha yako na Watu wengine Barabarani”.