Wakazi kitangili waiomba serikali kuchukua hatua za haraka dhidi ya fisi wala watu

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Wakazi wa Kata ya Kitangili katika Manispaa ya Shinyanga wamewaomba viongozi wa ngazi zote kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na matukio ya Fisi kushambulia watoto na kisha kuwasababishia vifo.

Diwani wa kata ya Kitangili Mariam Nyangaka

Wameyasema hayo leo wakati wa maombolezo ya kifo cha mtoto Albert Shija mwenye umri wa miaka 2 na miezi 10 aliyeuawa kwa kushambuliwa na Fisi juzi Jumamosi majira ya saa moja usiku katika mtaa wa Imalilo kata ya Kitangili.

Wananchi hao wamesema matukio ya watoto kuuawa na Fisi yameongezeka hali inayosababisha hofu na taharuki kubwa kwa wakazi hao ambao wameomba mamlaka husika zichukue hatua za haraka ili kukabiliana na hali hiyo inayotishia usalama

Diwani wa kata ya Kitangili Mhe. Mariam Nyangaka amekiri kuwepo kwa taharuki inayosababishwa na matukio hayo ambapo ameeleza kuwa ameitisha kikao maalumu kitakachohusisha makundi mbalimbali ya wadau watakaojadili jinsi ya kutatua changamoto hiyo.

“Hatua za moja kwa moja ni kwamba kesho tunakutana na wazee maarufu, viongozi wa dini, wazee wa mila tutawashirikisha kila nzengo tutakutana nao tujaribu kuangalia namna ya kutatua suala hili tunafanyaje ili wananchi wakae kwa amani”

Diwani huyo ametoa wito kwa wananchi wa Kata ya Kitangili kuchukua tahadhari ya kuwalinda watoto dhidi ya mazingira hatarishi ili kuwaepusha na matukio ya aina hiyo.

“wazazi tuwe makini kuwalinda watoto wetu hasa muda wa jioni kuanzia Saa 12 mzazi uhakikishe mtoto yupo nyumban lakini pia wazazi wawe na namba za simu za viongozi kingine wananchi wawe na vitendea kazi mfano vipenga au panga vitu ambavyo wataweza kujihami”

Kwa upande wa Idara ya maliasili, misitu na nyuki ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kushirikiana na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA kanda ya Mwanza wameanza operesheni maalumu ya kuwasaka wanyamapori aina ya Fisi ili kuthibiti matukio ya vifo na majeruhi.

Afisa misitu wa Halmashauri ya Manispaa James Mduma amesema kuwa operation hiyo imeanza kufuatia mfululizo wa matukio ya Fisi kujeruhi na kuua katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga ikiwemo kata ya Kitangili.

Mduma amefafanua zaidi kuwa utekelezaji wa operesheni hiyo unafanyika kwa kushirikiana na maafisa wa mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA kanda ya Mwanza.

“Naamini tunaweza tukafanya vizuri tukishirikiana na taasisi ya wanyamapori TAWA tumekwisha kuwa na mawasiliano nao lakini kwa matukio haya mawili wamekuja na hata sasa tuko nao wanaendelea na operation kwa maana ya kwamba tuwasake hao fisi wanaofanya hayo matukio kwa hiyo tukishirikiana na ofisi ya wanyamapori litadhibitiwa na ndiyo maana tunafanya kazi kwa kushirikiana nao vizuri” 

Akizungumzia suala hilo Afisa Mhifadhi wanyamapori Daraja la Pili kutoka kikosi dhidi ya ujangili, Mwanza Mohamed Mpoto mmoja kati ya Askari wanaoendesha msako dhidi ya Fisi huyo amefafanua kuhusu sheria ya wanyamapori inayohusisha madhara yatokanayo na mazingira hatarishi ya wanyama wakali.

“Sheria namba tano (5) ya mwaka 2009 ya wanyamapori imeainisha  wanyamapori wakali na wahalifu na mmoja wapo ni fisi. Kwa  kulitambua hilo sheria imeainisha madhara yoyote ambayo atasababishiwa mwananchi aidha kuuawa au kujeruhiwa kutatolewa kifuta machozi ambapo mtu akifa inatolewa shilingi Mil 1, majeruhi shilingi 500,000, Ng’ombe mmoja ni shilingi elfu 50 Mbuzi ni elfu25

Opareisheni hiyo inayoendelea katika Manispaa ya Shinyanga inafuatia kukithiri kwa matukio  ya kuuawa na kujeruhiwa kwa wananchi hasa watoto wadogo katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha mwaka huu 2021.