Mganga mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt Silvia Mamkwe akifunga mdahalo wa wanafunzi na vijana balehe |
Na Seif Mangwangi, Arusha
Tatizo la ugumba kwa wanaume na wanawake walio katika umri mdogo limeelezwa kuendelea kuwa kubwa nchini na ambalo limekuwa likisababishwa na ulaji wa mara kwa mara wa vyakula kama Chips pamoja na vyakula vilivyoondolewa madini muhimu.
Ili kudhibiti hali hii, wazazi na walezi nchini wametakiwa kuzingatia chakula chenye lishe kwa vijana wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe ili kuwajenga kiakili na mwili na kuwaepusha na maradhi yasiyoambukiza.
Akizungumza wakati wa kufunga mdahalo wa watoto wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe kuhusu mifumo ya chakula, ulioandaliwa na taasisi ya serikali ya Chakula na Lishe, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dk.Silvia Mamkwe amesema hali ya afya kwa watoto wadogo hivi sasa ni ya hatari sana.
Amesema wazazi wengi hujisahau na kuwapa watoto wao vyakula visivyokuwa na tija wakiamini wanawapenda sana watoto wao na badala yake ni kuwasababishia udumavu na upungufu wa damu kwa baadhi yao.
Dkt Mamkwe amesema katika utafiti uliofanywa nchini kati ya watoto 100 watoto 34 wanaugua tatizo la upungufu wa damu huku kati ya watoto100 watoto 25 wanakabiliwa na tatizo la udumavu na kuwasababishia kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kuhimili masomo.
“utafiti unaonyesha kuna hali ya hatari sana ya kiafya kwa watoto wetu, kati ya kila watoto 100 shuleni, watoto 34 wanakabiliwa na upungufu wa damu,kila kwenye watoto 100 watoto 25 wanakabiliwa na udumavu na kila kwenye idadi ya watoto 100 watano wanauzito uliozidi,”amesema.
Amesema hali hiyo inachangiwa na changamoto mbalimbali za mfumo wa uzalishaji,uhifadhi na usindikaji wa chakula,masuala ya masoko,upatikanaji wa chakula na ulaji usiofaa.
Dk.Silvia amesema hali si nzuri kwa maeneo ya vijijini hivyo kuna haja ya kuhamasishana na kusabambaza elimu ya lishe kwenye jamii ili wazazi na walevi wabadilike.
Mkurugenzi wa taasisi ya chakula na Lishe Dkt Germany Leyna akizungumza na waandishi wa habari katika mdahalo huo |
“Wengi tunafurahi kumpa mtoto chips ni kumpenda kijana au mtoto kumbe tunamuharibu na matokeo yake anapokuwa kijana anakosa nguvu za kuzaa na tunaishia kununulia dawa za kuongeza nguvu wakati ukimpa chakula lishe anajengeka kiafaya,akili na mwili,”amesema.
Wanafunzi na wazazi wakisikiliza hotuba ya mganga mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt Silvia Mamkwe |
Amesema kutokana na kuona ongezeko la udumavu na upungufu wa damu kwa watoto wenye umri wa kwenda shule na vijana balehe, wameamua kuendesha mdahalo huo na kukusanya baadhi ya vijana pamoja na wazazi wao,toka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani ili kutoa elimu ya masuala ya lishe.