Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo imekabidhi vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu mbalimbali msaada ambao ulitolewa na mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia kazi vijana na ajira Patrobas Katambi
Jumla ya watu 42 wenye ulemavu mbalimbali wamekabidhiwa vifaa hivyo katika ofisi za shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA Mkoa wa Shinyanga
Akikabidhi vifaa hivyo kwa wenye ulemavu wa viungo na wasioona Afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Shinyanga Elizabeth Mweyo ametoa Baiskeli 6 zenye magurudumu matatu za watu wenye ulemavu, fimbo nyeupe 20 kwa ajili ya wasioona pamoja na magongo 16 ya kutembelea wenye ulemavu, ambapo amewasisitiza walengwa kutobadili matumizi yaliyokusudiwa katika vifaa hivyo
“Kuna baadhi huwa mnapewa Baiskeli mnaenda kuziuza hamjapewa kwahiyo sababu mmepewa kwa sababu ya kuwasaidia ziwarahisishie kufanya majukumu yenu ya kila siku kwahiyo msiende kuziuza tutawafuatilia kwa sababu orodha yenu tunayo tutawafuatilia kujua hivyo vifaa mnavitumia, mnazo, zinafanya kazi au mmeshaziuza”
Baada ya kupokea msaada huo baadhi ya watu wenye ulemavu waliopatiwa vifaa hivyo wamemshukuru mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi vijana na ajira Patrobas Katambi na serikali kwa ujumla
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha walemavu Mkoa wa Shinyanga Bwana Mohamed Ally amewataka wale wote waliobahatika kupata msaada huo kuvitunza vifaa hivyo saidizi ili viweze kudumu
Naye mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA mkoa wa Shinyanga Richard Mpongo amewaomba watu wenye ulemavu kushirikiana na vyama vyao vyote pamoja na kujitokeza watu wenye ulemavu ambao hawatambuliki kwenye vyama