Wahitimu kidato cha nne watakiwa kufaulu ili kujihakikishia nafasi kidato cha tano

 Na  Mapuli  Misalaba, Shinyanga

Wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu kidato cha Nne Mwaka huu 2021katika  Shule ya Sekondari uhuru iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuwa na malengo ya kupata ufaulu mzuri kwenye mitihani yao ili kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindani katika soko la elimu.

Kauli hiyo imetolewa na wakili wa kujitegemea Ipilinga Panya Idebe ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 28 ya kidato cha Nne katika shule ya Sekondari Uhuru ambapo amesema wajibu mkubwa kwa wanafunzi hao ni kupata ufaulu mzuri 

“Nawaasa wanafunzi hasa wa kidato cha nne ili uweze kufaulu mtihani ni lazima uelewe falsafa ya  namna gani nzuri ya kuelewa masomo na kufaulu, ni lazima mjiandae vyema  kushinda ,mpange kushinda na mwisho mtarajie ushindi”

Akizungumza katika hafla hiyo mkuu wa shule ya Uhuru Sekondari Victoria  Nakiliaumi amesema licha ya hatua kubwa ya mafanikio lakini zipo changamoto kadhaa zinazohitaji kutatuliwa ikiwemo upungufu wa matundu ya vyoo kwa walimu

 “Shule yetu imekuwa na mafanikio makubwa sana lakini bado inakabiliwa na changamoto ambazo tukizipunguza tutadhidi kuwa na ufanisi zaidi kitaaluma baadhi ya changamoto tumeshawasilisha ofisi ya mkurugenzi kwa ajili ya kutatuliwa mfano upungufu wa walimu na baadhi ya masomo kuwa na upungufu wa vitabu tunaamini serikali itakapopanga walimu na sisi tutapata pia umaliziaji wa jengo la maabara la Biolojia lakini changamoto ambayo tunaileta kwako mgeni rasmi ni ukosefu wa matundu mawili ya vyoo vya walimu ya nje tunaamini utaendelea kutusaidia kadri utakavyojaliwa pia tunamatumani jinsi changamoto zinavyopungua ndivyo taaluma inazidi kupanda”

Baadhi ya  wanafunzi wanaohitimu  kidato cha nne mwaka huu 2021 wameeleza  kuwa siri kubwa ya mafanikio hayo ni uadilifu, upendo na ushirikiano

Wamesema kuwa katika kipindi chote ambacho wamekuwa katika mazingira ya shule walimtumainia  Mungu zaidi, lakini pia nidhamu kwa walimu, wazazi na jamii inayowazunguka

Mmoja wa walimu katika shule hiyo Mwalimu Wilbert Zungu amewaasa wanafunzi wanaobaki kuwa watiifu, wanyenyekevu, na wavumilivu ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wazazi na walimu kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo ili ziweze kutatuliwa

“Nipende kuwashauri wanafunzi wanaoendelea kubaki hapa wazingatie maelekezo ya walimu kwanza wawaheshimu wazazi na kuwasaidia kazi nyumbani lakini waje shuleni kwa wakati watimize jukumu lao la uanafunzi kazi ni nyingi wafanye na wasome kwa bidii watakutana na changamoto nyingi wavumilie kikubwa wawe karibu na walimu wao hasa walezi wa madarasa wanaweza kubaini changamoto zao na kuwa msaada wa karibu kwa namna yoyote ile”

Shule hiyo imefanya mahafali yake ya 28 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1990  ikiwa na wanafunzi 80 na kwamba mpaka sasa ina idadi jumla ya wanafunzi 829, kati yao  kidato cha Nne ni 187 wasichana 89 na wavulana 95