Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji, Geoffrey Mwambe amelitaka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), kufanya tafiti kuhusiana na suala la mitaji na masuala ya riba hali ambayo itasaidia kuonyesha namna mitaji inavyoweza kupatikana, athari za riba kubwa na njia za kusaidia kuzipunguza kama namna ya kuwawezesha Watanzania kuimarika kiuchumi.
Mwambe ameyasema hayo wakati alipokutana na kuzungumza na Bodi pamoja na Menejimenti ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi jijini Dodoma. Aidha, amefafanua kuwa sera ya uwezeshaji ni mtambuka na inamhusu kila mtu na sekta zote hivyo kuna umuhimu wa Baraza kuwaelewesha wananchi na kila sekta ili watambue kuwa wanalo jukumu la kuitekeleza sera hiyo.
Amefafanua Baraza lina kazi kubwa ya kuwalea wajasiriamali wanaofanya vizuri na kutoa ajira kwa watu wengine. Amesiistiza kuwa wapewe ushauri na kuwapendekeza kupata mikopo nafuu na kusaidiwa vitendea vya kisasa ili kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa wananchi wengi.
Awali akiongea katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa amebainisha kuwa mipango ya Baraza hilo ni kuhakikisha inafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wananchi kwa kuandaa sera ya Taifa ya ushiriki wa watanzania katika Uwekezaji na miradi ya kimkakati kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu,
Ameongeza kuwa Mipango ya Baraza hilo ni kuendeleza vituo vya uwezeshaji katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri, kuratibu utendaji wa jukwaa la wanawake kiuchumi katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri na ujenzi wa jengo la Ofisi kwa ajili ya matumizi ya Baraza.
Kwa niaba ya Bodi ya Baraza, Prof. Lucian Msambichaka alimhakikishaia alimshukuru Mhe. Waziri kuwa maelekezo aliyoyatoa watayatekeleza kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwezeshaji Prof. Godius Kahyarara Pamoja na Watumidhi wa Idara ya Uwezeshaji Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji.