Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde amewataka walimu wa Dodoma Jiji kupitia kupitia kitengo cha KE, ndani ya Chama cha Walimu Tanzania(CWT) kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi kwa lengo la kurahisisha uratibu wa shughuli za kila siku za kitengo hicho.
Mbunge Mavunde ameyasema hayo jana katika ukumbi mdogo wa Jakaya Kikwete Convention Centre wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani ambapo ametumia fursa hiyo kuwapongeza walimu wote wa Dodoma Jiji kwa kazi nzuri sana wanayoifanya katika kuwalea na kuwaelimisha wanafunzi wa Dodoma Jiji.
“Ninawapongeza sana walimu wote wa Dodoma Jiji kwa kazi nzuri mnayoifanya katika ulezi na uelimishwaji wa wanafunzi wetu,tuendelee kuifanya kazi hii ya kitume ili kulijenga taarifa lenye maadili na maarifa makubwa.
Kwakuwa mmeleta ombi kwangu la kusaidia miradi ya kiuchumi,kwa upande wangu kama Mbunge nitawanunulia shamba ekari 1 lililopo karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga. Ni lazima sasa kitengo KE mje na mipango mbalimbali na kubuni miradi ya kiuchumi inayoendana na Dodoma ya leo”Alisema Mavunde
Katika kuendelea kuwapa motisha walimu wake,Mbunge Mavunde amechangia Tsh 2,000,0000 kwa ajili ya safari ya kwenda Mbuga za Wanyama za Ruaha,Iringa ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kukuza Utalii wa ndani ambapo mwaka 2019 walimu hao pamoja na Mbunge Mavunde walitembelea katika michoro ya mapangoni Kondoa.