Serikali yaagiza kamati za ulinzi na usalama wa mtoto ziimarishwe

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiangalia boksi la chaki zinazotengemezwa na kikundi Cha Wanawake Cha Huyandola kilichopo Wilayani Mbeya, alipotembelea kikundi hicho kujionea shughuli zinazofanywa na kikundi hicho.
Mmoja wa wanakikundi za ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto katika Kata ya Ilanya, Wilayani Mbeya, Joyce Mwakimenya akimueleza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis namna wanavyowafudisha watoto kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Meneja wa Kituo cha maadilisho cha Irambo, Mbeya Justine Mjema akipokea zawadi kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipotembelea kituo hicho .
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwasalimia watoto wa shule ya Msingi ya Maadilisho iliyopo kata ya Irambo, Wilaya ya Mbeya baada ya kufanya ziara shuleni hapo

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (WAMJW)

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameagiza kuimarishwa kwa  Kamati za ulinzi na usalama wa mtoto ili zitumike kukabiliana vitendo vya ukatili.

Naibu Waziri huyo ametoa agizo hilo mkoani Mbeya wakati akizungumza na Kamati za ulinzi wa mwanamke na mtoto pamoja kikundi cha malezi chanya zinazotekeleza Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili wa Wanawake na watoto katika Halmashauri ya Mbeya

” Uzoefu unaonesha maeneo vilipo vikundi hivi vya malezi vimekuwa na mchango mkubwa katika kuzuia ukatili na kutoa msaada kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, nitoe rai kwa  watendaji wa ngazi zote washirikiane na kamati za MTAKUWWA kuhakikisha masuala haya yanayogusa Wanawake na watoto yanashughulikiwa kikamilifu,” amesema Mwanaidi.

Wakitoa taarifa ya MTAKUWWA kwa niaba ya wenzake Fransisco Mgwira amesema wamefanikiwa  kupunguza vitendo vya ukatili kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine ikiwemo uongozi wa Kata.

“Kamati imefanikiwa kutoa elimu ya ulinzi na usalama dhidi ya ukatili kwa watoto na wanawake katika shule za msingi na Sekondari pamoja na kutambua mazingira hatarishi kwa watoto na kutoa maelekezo kwa viongozi namna ya kuwakinga watoto” amesema Fransisco Mgwira.

Mhe. Mwanaidi pia ametoa wito kwa mamlaka zinazosimamia kesi za ukatili dhidi ya watoto na wanawake musimamia uharakishaji wa kesi hizo na waathirika wapate haki zao. 

Naibu Waziri Mwanaidi amesema kesi hizo za ukatili zikiachwa muda mrefu, zinapoteza ushahidi hivyo wahusika wanakosa haki zao zinazostahili na kuzidi kuathirika kisaikolojia na kufanya jitihada za kutokomeza vitendo hivyo kusuasua.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Mwanaidi amewataka wazazi kushirikiana katika malezi na kuwajibika ili kuwalinda watoto ili kutofikia hatua ya kukinzana na Sheria.

Awali akiwasilisha taarifa ya shule hiyo ya maadilisho, msimamizi Justin Mjema amesema sababu kubwa za watoto kufikia hali ya kukinzana na Sheria na hatimaye kupelekwa shuleni hapo ni migogoro ya familia, ndoa zilizovunjika au wazazi kutotimiza majukumu yao.

Aidha, Mhe. Mwanaidi akiwa katika Hamashauri ya Wilaya ya Mbeya ametembelea na kuona shughuli zinazofanywa na kikundi cha akina mama wajasiriamali cha Huyandola kinachojihusha na kutengeneza chaki ambapo ameiagiza Halmashauri kuzidi kukiwezesha kwa kukitafutia soko ili kiweze kurejesha mkopo walioupata.