Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Nyehunge iliyoko wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, Lucas Moshi anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuchoma mabweni ya shule hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Sanyi Ganga ameyasema hayo Septemba 29, 2021 baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea uharibufu mkubwa na vifaa vya wanafunzi uliosababishwa na moto huo uliotokea Septemba 27 mwaka huu.
DC Ganga amesema mabweni mawili ya shule hiyo iliyopo katika halmashauri ya Buchosa yanayotumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano na sita yaliungua moto, hivyo wanafunzi hao kuhamishiwa chumba kimoja cha darasa kwa ajili kulala.
Amesema kabla ya mwanafunzi huyo kusimamishwa, alisimamishwa masomo na kutakiwa kufika shuleni na wazazi, lakini hakufanya hivyo, badala yake alikuwa akizunguka maeneo ya shule.
Mkuu wa shule hiyo, Adofu Domician amesema tukio hilo ambalo limetokea mara mbili kwa muda wa siku mbili limemshtua na kuomba Serikali ifanye uchunguzi kwa kina na kusaidia shule hiyo.
Amesema hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa Wala kupoteza maisha, mbali ya mali za wanafunzi zilizoteketea kwa moto zikiwemo nguo, madaftari pamoja na magodoro na kuiomba Serikali pamoja na wadau wa elimu kujitokeza kusaidia wanafunzi hao.
Amesema siku ya tukio, mwanafunzi huyo alikuwepo eneo la shule na ndipo alipokamatwa kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano na Polisi.