Na Mwandishi Wetu
MTANDAO wa shule saba za St Anne Marie Academy umetangaza kwamba kuanzia sasa hakuna mwanafunzi atakayefukuzwa shule baada ya mzazi wake kufariki na kushindwa kulipa ada ya kuendelea na masomo.
Uamuzi huo ulitangazwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa shule hizo ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Dk. Jasson Rweikzia, wakati wa mahafli ya 14 ya moja ya shule zake ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
Mbali na Sunshine shule zingine zilizoko chini ya St Anne Marie Academy ni Sekondari ya Brilliant, Rweikiza Nursery and Primary na St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri .
wa shule za St Anne Marie Academy zinazomiliki shule hiyo ya Sunshine ya Kibaha akilishwa keki na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo kwenye mahafali yaliyofanyika Jumamosi shuleni hapo |
” Tumekuwa tukipoteza wazazi wengi na mwezi huu pekee tumepoteza wazazi watatu na hali hii imekuwa ikiathiri sana wanafunzi kitaaluma na wengine kuacha shule kwa kushindwa kulipa ada lakini kuanzia sasa hakuna atakayefukuzwa shule kwa kukosa ada baada ya mzazi wake kufariki,” alisema
” Kama yuko darasa la kwanza na amefiwa na mzazi wake ataendelea kusoma mpaka darasa la saba na kama ni sekondari ataendelea mpaka kidato cha nne,” alisema Dk. Rweikiza
Dk. Rweikiza alisema katika mpango wa kuinua taaluma shuleni hapo wameaandaa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu kwa awatakaofanya vizuri kwenye masomo yao na ziara za kimasomo kwenye mbuga mbalimbali za wanyama.
Amesema mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza atapata sh 600,000 na atakayepata daraja la II atapata Sh 200,000 na kwamba lengo ni kuhakikisha hakuna daraja la nne wala daraja la tatu shuleni hapo.
Mkuu wa shule ya Sunshine, Frank Raphael alisema wahitimu hao wameandaliwa vizuri kitaaluma na wanatarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
Amesema wanafunzi hao wamewezeshwa kufikia hapo na walimu wenye taaluma na uzoefu wa kutosha huku akimshukuru Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Rweikiza kwa kuendelea kufanya maboresho.
Pia amesema Dk. Rweikiza amewawezesha kupata maabara iliyosheheni vifaa vya kutosha, vifaa vya kufundishia kama vitabu, projekta, mashine ya kudurufia, maji safi, ulinzi na huduma bora za afya.
Kwenye maonyesho ya kitaaluma shuleni hapo wahitimu wa kidato cha nne wa shule ya Sunshine walitia fora kwa namna walivyoweza kuelezea masomo ya baiolojia na uhandisi wa umeme kana kwamba ni wakufunzi waliokwisha kuhitimu kwenye masomo hayo.