*rais samia; kipindi cha miezi sita wawekezaji wamevunja rekodi ya kuitikia wito wa kuja kuweza nchini *

Na. OWM-UWEKEZAJI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha miezi Sita ikiwa ni kuanzia mwezi Machi hadi Agosti, 2021,  Idadi ya Wawekezaji wanye nia ya kutaka kuweza nchini imeongezeka.

Mhe.  Rais Samia ameyasema hayo juzi 26 Septemba, 2021 wakati  akisalimiana na Wananchi wa Wilaya ya Dodoma Mjini  waliofika kumpokea  katika eneo la Chinangali mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Dodoma akitokea Jijini Dar es Salaam.   

Amefafanua kuwa kuna miradi ambayo hawakujua kuwa wawekezaji wanakuja  hivyo miradi hiyo itatekelezwa kama ilani ilivyo eleza na miradi mingine Ilani inaeleza wawekezaji watafutwe.

“Ilani ilitutuma tutafute wawekezaji waje kuwekeza, nami nataka kuwaambia kuwaambia wawekezaji tumepata wengi  mno. Lakini niwaambie kwamba katika kipindi cha miezi sita kumekuwa na idadi kubwa ya wawekezaji ambao wanataka kuwekeza Tanzania.  Kati ya hao tunakiwanda cha mbolea kinachoendelea kujengwa hapa Dodoma. Nawaahidi na wengine watakuja” Amesisitiza Mhe. Rais Samia.

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, M he.Geoffrey Mwambe, akiongea na vyombo vya Habari juu ya juhudi zinazofanywa na Ofisi hiyo,  pamoja na Taasisi zake katika kuweka Mazingira Wezeshi kwa wawekezaji nchini, aliutaja mradi wa uwekezaji wa kimkakati wa  Kampuni ya ITRACOM FERTILIZERS LIMITED unaotekelezwa katika mkoa wa Dodoma. 

Aliufafanua mradi huo kuwa Mradi huo utazalisha mbolea asilia. Mradi huo una mtaji wa Dola za Marekani milioni 180 na unatarajiwa kuzalisha ajira 3000. Mradi huo utaingiza fedha za kigeni, utaongeza kipato kwa wananchi na mapato ya serikali kupitia kodi. 

Mhe. Mwambe alibainisha kuwa Katika kipindi cha mwezi Machi hadi Agosti, 2021 jumla ya miradi 133 imesajiliwa ikilinganishwa na miradi 105 iliyosajiliwa katika kipindi hicho Mwaka 2020 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 27.  

Miradi iliyosajiliwa katika kipindi hicho inatarajiwa kuzalisha ajira 29,709 ikilinganishwa na ajira 8,252 zilizotarajiwa kuzalishwa katika kipindi hicho Mwaka 2020. Miradi hiyo ipo katika Sekta ya Kilimo, ujenzi/majengo ya biashara, nishati, Miundombinu ya kiuchumi, Taasisi za fedha, rasilimali watu, viwanda, usafirishaji, utalii na huduma. 

Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji  pamoja na Taasisi zake inaendelea kuwahakikishia wawekezaji kuwa itaendelea kuratibu masuala ya uwekezaji ili kuhakikisha wanakuwa na mazingira wezeshi ya uwekezaji.