Mbeya kuadhimisha siku ya unywaji maziwa kimataifa kwa kutoa misaada kwa vituo vya kulelea yatima

Katibu Tawala wa mkoa wa Mbeya,Dkt Angelina Lutambi akizungumzia shughuli zitakazofanyika kabla ya kuelekea siku ya maadhimisho ya kimataifa ya Unywaji wa maziwa mashuleni Septemba 29 mwaka huu.(Picha na Joachim Nyambo)


 Na Joachim Nyambo,Mbeya.

Katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kunywa maziwa mashuleni Septemba29, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, imepanga kutoa misaada kwenye vituo vya kulelea watoto yatima hususani walio na umri wa chini ya miaka mitano na katika wodi za wajawazito pamoja na watoto katika Hospitali.

Shughuli nyingine ni kutembelea na kutoa msaada kwenye magereza ya watoto ambapo kazi hizo zitafanyika Septemba 27 kabla ya Septemba 28 ambapo kutakuwa na kikao kitakachowakutanisha wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zote za mkoa wa Mbeya pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa na maadhimisho kamili yatakuwa katika viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya Septemba 29.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Katibu tawala mkoa wa Mbeya, Dk Angelina Lutambi alisema lengo kuu la kuwa na maadhimisho ya Siku ya unywaji maziwa mashuleni ni kukuza tabia ya unywaji wa maziwa na hivyo kupanua soko la bidhaa hiyo huku ikiimarisha afya za watu hususani watoto wadogo.

Dk Lutambi alifafanua kuwa kiwango cha matumizi ya maziwa na bidhaa zake bado ni kidogo ambapo hadi sasa inakadiriwa wastani wa unywaji kwa mtu mmoja kwa mwaka ni lita 54.7 wakati kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Chakula duniani(FAO) ni angalau lita 200 kwa mtu kwa mwaka.

“Hivyo tuna kazi kubwa ya kuhamasishana ili tufikie kiwango hicho kilichopendekezwa  kwa afya bora.Na tunasisitiza kuna umuhimu wa kuwa na program ya unywaji wa maziwa shuleni  ili kujenga tabia ya unywaji maziwa kwa watoto tangu wakiwa wadogo.”

“Kila jumatano ya mwisho wa mwezi wa tisa kila mwaka ilitengwa kuwa  siku maalumu ya kuadhimisha unywaji wa maziwa shuleni.Maziwa yana faida kubwa kiafya na kiuchumi.Yana virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini kwa afya bora.”

Aliitaja faida nyingine ya maziwa kuwa ni pamoja na kuboresha ukuaji wa watoto kwani  huimarisha mifupa,ukuaji wa akili na pia ukuaji kimwili na hivyo kuwezesha watoto kuwa na afya bora na pia kupata matokeo mazuri kitaaluma sambamba na kuanza mapema kuwa na tabia ya lishe bora.

Katibu Tawala huyo alisema hadi kufikia Septemba mwaka jana shule 210 nchini zenye jumla ya wanafunzi 89,922 zilinufaika na mpango wa kitaifa wa unywaji maziwa shuleni  katika mikoa 10.

Aliutaja mkoa wa Mbeya kuwa miongoni mwa mikoa hiyo na mingine ikiwa ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga,Dares salaam, Iringa, Njombe, Morogoro, Mwanza na Mara.

 

Alisema takribani Lita milioni 12 za maziwa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 19 zimetumika nchini katika  vipindi tofauti kuanzia mwaka 2006 hadi 2020.

Alisema kwa mwaka 2020/2021 programu za unywaji maziwa zimeendelea kutekelezwa katika  shule 30 nchini  kutoka shule 210 zilizokuwa zikitekeleza  mpango huo.

Aliitaja mikoa inayotekeleza mpango huo kwa sasa ni Kilimanjaro iliyo na shule 24,Iringa yenye shule mbili  na Mbeya yenye Shule nne ambapo programu inaendeshwa kwa ushirikiano wa wazazi na viwanda vilivyopo kwenye mikoa hiyo.

 

Kaulimbiu ya Siku ya unywaji wa maziwa mashuleni mwaka huu ni Faulu mtihani kwa glasi moja ya maziwa kila siku.