Na Mwandishi Wetu,Katavi
Mkoa wa Katavi umepokea zaidi ya shilingi bilioni 15 zitakazotumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijiji na Mijini (TARURA) mkoani humo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko |
Fedha hizo ni ongezeko la asilimia 150 ya bajeti ya miradi ya barabara kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2020/2021 ambapo mkoa huo ulipokea shilingi bilioni 6.1.fedha ambazo zilitumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara,madaraja na usimamizi.
Mwanamvua Mrindoko,Mkuu wa Mkoa wa Katavi amesema hayo jana katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda wakati akitoa taarifa kwenye ufunguzi wa kikao cha bodi ya barabara mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa kuongeza kwa fedha hizo zitatumika kwenye kuboresha miundombinu ya barabara iliyopo mkoani Katavi ili kuimarisha uchumi wa wananchi unaotegemea sekta ya barabara,ambapo barabara hutumika hasa kwenye kusafirishia mazao ya kilimo,bidhaa na kuruhusu watu kuingia na kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya mkoa.
Alisema juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ni utekelezaji wa miradi ya barabara kupitia kuleta fedha kwenye taasisi ya Tarura na Tanroad mkoa wa katavi ili kusaidia mkoa wa katavi kuinuka kiuchumi na kimaendeleo.
Aidha Mrindoko aliwataka Tarura kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara hasa kwenye kusimamia ubora wake ili kuendana na thamani ya fedha zinazotolewa na serikali,Huku akiwaomba wananchi kulinda barabara hizo kwa kutokujihusisha na uharibifu wa alama za barabarani na kutokupitisha mifungo kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Innocent Mlay,Mratibu wa Tarura Mkoa wa Katavi akiwasilisha mpango wa bajeti wa matengenezo ya barabara kwa mwaka fedha 2021/22 alisema fedha zilizoidhinishwa Tshs 15,321,975,829.08 ni kwa ajili ya utengenezaji wa barabara,madaraja na usimamizi.
Mlay alieleza kuwa mchanganuo wa fedha ni kwenye matengenezo ya barabara ni Tshs 4,386,975,829.08 na fedha za maendeleo ni Tshs 10,935,000,000/= ambapo wanufaika ni halmashauri za Nsimbo,Mpimbwe,Mlele,Tanganyika na Manispaa ya Mpanda.
Alieleza kuwa katika mpango huo wanatarajia kuzifanyia matengenezo barabara zenye jumla ya urefu wa km 658.89 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida,sehemu korofi,matengenezo ya muda maalumu pamoja na ujenzi wa madaraja madogo naya kati.
Akichangia hoja hiyo mbunge wa jimbo la Mpanda mjini Mkoa wa Katavi,Sebastiani Kapufi suala la Tarura kuimalisha usimamizi wa miradi ya ujenzi wa barabara ni muhimu,Kwani kuna baadhi ya wakandarasi wamekuwa sio waaminifu kwa kuchelewesha makusudi kutokukamilisha kwa wakati ujenzi wa miundombinu hiyo kitendo ambacho kinawachonganisha wananchi na serikali yao.
Vilevile ameishukuru serikali kwa kuidhinisha zaidi ya bilioni 15 kwa Tarura Mkoani Katavi na katika kuuga mkono kazi inayofanywa na rais Samia Suluhu Hassain ametoa greda ya kukwangua barabara pamoja na mafuta ya kuendesha mtambo huo ya kiasi cha shilingi mil 10.