Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda |
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Waziri wa kilimo Profesa ADOLF MKENDA leo ameitambulisha rasmi kamati maalumu ya kufuatilia mfumo wa ununuzi wa mazao ya jamii ya mikunde ghalani kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga
Amesema hatua ya kuundwa kwa tume hiyo imelenga kupata taarifa muhimu na kupokea maoni ya wadau wa kilimo wa Mkoa wa Shinyanga kuhusu maendeleo na changamoto zinazojitokeza katika mfumo wa ununuzi wa wa mazao jamii ya mikunde kwa mfumo huo wa stakabadhi ghalani.
“Leo tumekuja na timu ya kupitia mfumo wa mauzo ya Dengu,Choroko na Ufuta na hatua gani tunatakiwa tuchukue ili utaratibu wa stakabadhi ghalani ukitumika usiwe na buguza,
Timu hiyo inaongozwa na dkt Hamis Mwinyimvua akisaidiwa na dkt Anaclet Kashuliza,huku wajumbe wengine ni pamoja na dkt Luhinduka Remidius ,bwana Bamey Laseko,dkt Wihelm Ngasamiaku na bwana Emest Doriye”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Philemon Sengati amesema Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuhakikisha inaondoa changamoto katika tasnia ya kilimo.
“Tunataka tufanye kazi kama timu serikali ni moja na tunataka tuende pamoja katika masuala ya msingi ya ustawi na maendeleo ya Taifa letu Serikali ya Rais Samia kupitia wizara ya kilimo wamechukua hatua mbele kutuma hii tume ili kupata taarifa za msingi kuhusiana na maendeleo na changamoto za kimfumo wa ununuzi wa mazao ya jamii ya mikunde ili hatimaye waweze kuweka mapendekezo ambayo yatakuja na msimamo wa pamoja ambao ni endelevu,
Mimi pamoja na wakuu wa wilaya tuwahakikishie tutawapatia ushirikiano ili hii kazi ifanyike kwa ukamilifu wake na itoe tija kubwa iliyokusudiwa na serikali ya Rais Samia”